
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Katibu wa Wilaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, James Mgego, amesema kuwa mtumishi mwema ni yule anayewaletea wananchi matokeo chanya ya maendeleo.
Akizungumza mbele ya wanachama na wananchi, Mgego amesisitiza kuwa Ilani ni mkataba kati ya chama na wananchi, na kwamba utekelezaji wake umekuwa wa viwango vya juu kwa zaidi ya asilimia 90.
Mgego amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake wa huruma na mageuzi makubwa katika sekta za elimu, afya, na ruzuku za kilimo.
Aidha, amewapongeza viongozi wa kata ya Bombambili, akiwemo Diwani Jeremiah Mlembe na Diwani wa Viti Maalum kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa ushirikiano mkubwa, akiitaja kama kazi iliyotukuka kwa maendeleo ya wananchi.
Amesema kuwa ushahidi wa utekelezaji bora unaonekana katika miradi ya maendeleo iliyoletwa kwa wananchi wa Bombambili kupitia Ilani ya CCM.
Katika kuelekea uchaguzi mkuu, Katibu huyo amewataka wanachama kuwa wamoja, akieleza kuwa chama kina utaratibu mzuri unaohakikisha haki inatendeka kwa wote wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
Amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi na kuendelea kuwa na imani na chama hicho pamoja na kiongozi mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhihirisha kuwa na dhamira ya kweli ya kuwaletea watanzania maendeleo.
Mgego pia amewapongeza viongozi mbalimbali wa serikali na chama kwa mchango wao, akiwataja Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Oddo Mwisho, Mbunge Dkt. Damas Ndumbaro, Chifu Mbano na Mkurugenzi wa Manispaa Muhoja.
Amesema kuwa kwa pamoja wameonyesha mshikamano wa karibu na wananchi
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa watanzania kupuuza propaganda kama "No Reform No Election" na badala yake kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa CCM na Rais Samia ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Social Plugin