Naibu Meya Jeremiah Mlembe ambae ni diwani wa kata ya Bombambili Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma akionesha kitabu alichokiandaa kwa ajili ya mafanikio yaliyotekelezwa kwa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi CCM kwa kipindi cha miaka mitano 2020-2025 kata ya Bombambili
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Naibu Meya wa Manispaa na Diwani wa Kata ya Bombambili, Mheshimiwa Jeremiah Mlembe, ametaja mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano (2020-2025), ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo.
Mlembe amesema kuwa taarifa hii ni sehemu ya utaratibu wa serikali kusoma utekelezaji wa ilani ya CCM kila mwaka wa fedha, kwa kuwa CCM ndicho chama tawala na kinachotoa dira ya utekelezaji wa shughuli za serikali.
Kata ya Bombambili ina mitaa mitano na kwa mujibu wa Sensa ya 2022, ina wakazi 25,130 wakiwemo wanawake 13,518 na wanaume 11,612 wakiwa katika kaya 7,750.
Katika sekta ya elimu, utekelezaji mkubwa umeonekana kupitia ujenzi wa shule mpya za sekondari na msingi ikiwemo Bombambili Sekondari, Mputa, Tembo Mashujaa, Sokoine na Chandamali.
Aidha, jumla ya madawati 140 yamenunuliwa na kusambazwa katika shule za msingi ili kupunguza uhaba wa madawati.
Kwa upande wa miundombinu, barabara ya lami yenye urefu wa km 1.8 na taa za barabarani 48 zimejengwa kuanzia Uwanja–Bombambili hadi Mwembechai Matarawe.
TARURA imechangia zaidi kwa kutoa shilingi milioni 517 kwa ajili ya daraja na barabara ya kiwango cha lami kutoka Sanga One hadi Bohari (km 0.9) pamoja na uchongaji na upanuzi wa mtandao wa barabara mpya wenye urefu wa km 8.3.
Pia, Mheshimiwa Mlembe ameeleza kuwa utekelezaji huo umehusisha miradi ya vivuko, masoko, TASAF, afya na lishe – jambo linaloonesha dhamira ya kweli ya kutatua changamoto za wananchi.
Ametoa wito kwa jamii kuwapa moyo viongozi wanaofanya kazi kwa bidii, kwani kazi hiyo ni ngumu
Msafir Abdala Omari amezungumza kwa niaba ya wananchi, ameipongeza serikali na Mheshimiwa diwani Mlembe kwa utekelezaji mzuri wa kazi zilizofanywa kwa ilani ya chama cha mapinduzi CCM
Wananchi hao wameonyesha imani yao kubwa kwa diwani huyo kwa kuchangia fedha taslimu shilingi 74,000 kwa ajili ya kumsaidia kuchukua fomu ya kugombea tena nafasi ya udiwani mwaka 2025, wakisisitiza kuwa bado wanahitaji uongozi wake madhubuti.
Zahanati ya Bombambili
Social Plugin