
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Katika kuadhimisha Siku ya Wajane Duniani, mkoa wa Mtwara umefanya maadhimisho maalum leo tarehe 23 Juni 2025 katika ukumbi wa Mustafa Sabodo, ukilenga kuzungumzia changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wajane, ikiwa ni pamoja na upweke, unyanyasaji wa kijamii na changamoto za kiuchumi.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Rechal Kasanda, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala.
Akizungumza kwa msisitizo, Rechal amelaani vikali vitendo vya ukatili ndani ya ndoa na kusema kuwa hakuna ndoa yenye wosia maalum bali kila wanandoa wana mtindo wao wa kuishi.
Ametoa wito kwa jamii kuacha kuwaambia watoto wavumilie ndoa zenye manyanyaso kwani mara nyingine mtu anayeonekana kuvumilika huenda ni muuaji wa taratibu.
Amesisitiza kuwa mwanamke ana thamani sawa na mwanaume na kwamba wanawake wa sasa wanafanya mambo makubwa katika jamii, ikiwemo kulea familia kwa uadilifu na kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na ya kumcha Mungu.
Kwa upande wa wajane kupitia Bi Zainabu Mohamed wamewasilisha kilio chao akieleza namna wanavyokumbwa na changamoto baada ya kufiwa na waume zao.
Amesema baadhi ya wajane huingia kwenye msongo wa mawazo, sonona, na magonjwa mbalimbali kutokana na upweke na mila potofu zinazoendelea kuwabagua.
Ameeleza jinsi ambavyo wajane husingiziwa kuwa chanzo cha vifo vya waume zao, kunyimwa mirathi, na kuachwa wakihangaika kusimamia malezi na elimu ya watoto wao.
Aidha, Bi Zainabu ametoa wito kwa serikali na jamii kuwapa kipaumbele wajane hasa kwenye huduma za afya, elimu kwa watoto wao na fursa za kiuchumi.
Ameongeza kuwa kupitia chama cha wajane, wameamua kujipanga na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao, ambapo amewahamasisha wajane wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili wawe sauti ya mabadiliko.
Maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa matumaini na ujasiri kwa wajane, huku wito mkubwa ukitolewa kwa viongozi wa serikali, wanajamii, na mashirika binafsi kuwaunga mkono wajane ili waweze kuishi maisha yenye heshima, utu na maendeleo.
Ujumbe huo umeeleza kuwa huu ni wakati muafaka wa kuvunja ukimya na kukomesha mila kandamizi zinazowanyima wanawake haki zao pindi wanapopoteza wenza wao.

Mkuu wa wilaya ya masasi mh Rachel kasanda akiwa na baadhi ya wajane ambao walifika na bidhaa zao kama mojawapo ya biashara wanazozifanya katika vikundi vyao vya wajane mkoani Mtwara
Social Plugin