Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC BATILDA KUONGOZA JUKWAA LA SABA LA VYAMA USHIRIKA TANGA


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi  Dkt. Batilda Salha Burian
Mwenyekiti wa Jukwaa la saba la vyama vya ushirika Dkt. Godwin Maimu, (Dkt Abbas Kombolela)

Na Hadija Bagasha -  Tanga

Wanaushirika pamoja na wadau zaidi ya 500 wanatarajiwa kulitumia jukwaa la saba la vyama vya ushirika kuibua fursa mbalimbali na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo, hali itakayosaidia ukuaji wa uchumi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi  Dkt. Batilda Salha Burian wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, kuelekea jukwaa hilo litakalofanyika Juni 4 hadi 6 mwaka huu, katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Balozi Dkt. Batilda amesema kuwa jukwaa hilo ni la saba tangu kuanzishwa kwake kufuatia wazo lililozaliwa na wanaushirika waliokutana kwenye kongamano la ushirika lililofanyika mwaka 2016 jijini Dodoma.

“Lengo kuu la jukwaa hili ni kutangaza bidhaa zinazozalishwa na wanaushirika, kuwakutanisha pamoja na kujadili maendeleo ya sekta ya ushirika. Tunafurahia kuwa hadi sasa tuna benki ya ushirika, jambo ambalo ni mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita,” alisema Dkt. Buriani.

Ameongeza kuwa jukwaa hilo litashirikisha vyama vya ushirika ikiwemo SACOS, AMCOS, viwanda, sekta ya maziwa, uvuvi na madini. Pia vyama vikuu vya ushirika vitakavyounganisha vyama vya msingi pamoja na watoa huduma kama mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), mashirika ya umma na sekta binafsi watashiriki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Dkt. Godwin Maimu, (Dkt Abbas Kombolela)  alisema kuwa jukwaa hilo litatoa fursa kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wa ndani na nje ya nchi, kujifunza mambo mengi kuhusu ushirika ambayo hayajulikani kwa wengi.

“Rai yangu kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na mikoa jirani ni kuja kwa wingi kuona fursa zilizopo Tanga. Kama kawaida yetu tunasema ‘Tanga wajaleo kuondoka majaliwa,’ kwa sababu kuna fursa za kipekee ambazo hazipatikani mahali pengine,” aliongeza Dkt. Maimu.

Naye Mrajisi msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tanga, John Henjewele, alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa namna anavyoendeleza ushirika na kuhakikisha shughuli zake zinafanyika bila changamoto.

Aidha, aliwahimiza vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za vyama vya ushirika kwa kuwa ni njia mojawapo ya kujikwamua na changamoto za ajira na maendeleo.

“Vyama vya ushirika ni sehemu pekee yenye fursa za ajira na maendeleo. Naomba vijana walione ushirika kama sehemu yao ya kuchangamkia masuala ya kiuchumi,” alisema Henjewele.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika jukwaa hilo ni pamoja na kuhamasisha unywaji wa maziwa baada ya takwimu kuonesha kuwa jamii bado haijajenga utamaduni wa unywaji wa maziwa kwa kiwango kinachotakiwa.

Jukwaa la saba la ushirika linatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha vyama vya ushirika nchini kwa kuviboresha na kuwaunganisha na wadau mbalimbali. Kupitia jukwaa hili, fursa zilizojificha katika sekta ya ushirika zitafunguliwa, na hivyo kusaidia kuinua maisha ya Watanzania kiuchumi. Ni wajibu wa kila mdau kuchangamkia fursa hizi kwa maendeleo endelevu ya taifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com