Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU 28 WAFARIKI KWA AJALI MBEYA,SERIKALI YACHUKUA HATUA



Watu 28 wamefariki dunia na wengine 8 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika eneo la Mlima Iwambi, Barabara Kuu ya Tanzania-Zambia, mkoani Mbeya. 

Ajali hiyo imehusisha lori lenye namba za usajili T.830 EDP na T.148 CTD, ambalo lilifeli breki na kugonga magari mawili—daladala na gari dogo aina ya Kirikuu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za pole kwa familia za wafiwa, majeruhi na wananchi wa Mbeya kwa ujumla. Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Rais Samia amesema:

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya ndugu zetu 28 na majeruhi 8... Ninawaombea marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone haraka.”

Aidha, Rais Samia ameagiza Jeshi la Polisi kuimarisha usimamizi wa sheria za usalama barabarani, pamoja na TANROADS na TARURA kuboresha miundombinu ya barabara hasa katika maeneo hatarishi.

Katika hatua za haraka, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dkt. Juma Zuberi Homera, ameiagiza TANROADS kuharakisha ujenzi wa barabara ya mchepuo kutoka Mbalizi hadi Iyunga, ili magari makubwa yaepushe kutumia barabara ya sasa inayokabiliwa na msongamano mkubwa. 

Dkt. Homera amesema kuwa agizo hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia ili kupunguza ajali zinazohusisha magari makubwa.

Serikali imesema itagharamia matibabu ya majeruhi wote waliolazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi, pamoja na kutoa rambirambi ya shilingi 500,000 kwa kila familia iliyopoteza mpendwa wao. Pia, maandalizi ya majeneza kwa miili yote 28 yatasimamiwa kikamilifu na serikali.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amethibitisha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva wa lori, ambaye licha ya kuwa amejeruhiwa, anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi. 

Amewataka madereva wote nchini kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com