Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUTANO MKUU WA 23 WA MBIFACU WAFANYIKA MBINGA, RUVUMA

Wajumbe wakipiga picha na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Peres Magiri
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Peres Magiri akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Chama cha Ushirika MBIFACU
Mkuu wa Wilaya wa Nyasa Peres Magiri wa tatu kushoto akiwa katika Picha ya pamoja na viongozi wa Chama cha Ushirika baada ya kutoka katika Mkutano Maalum wa wa kawaida wa 23 wa mwaka wa wanachama wa MBIFACU

Na Regina Ndumbaro Mbinga-Ruvuma

Mkutano Mkuu wa kawaida wa 23 wa mwaka wa wanachama wa Mbinga Farmers’ Cooperative Union (MBIFACU) umefanyika leo, tarehe 8 Mei 2025, katika ukumbi wa Jimbo Katoliki, Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma.

Mkutano huo umefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Maamuzi ya pamoja, nguvu ya maendeleo ya Mbifacu” na umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wanachama na wadau wa ushirika.

Mgeni rasmi katika Mkutano huo ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed.

Katika hotuba yake, Magiri amewapongeza viongozi wa MBIFACU kwa juhudi zao za kusimamia ushirika na maendeleo ya wanachama.

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuwajali wananchi, hususan wakulima, na kwa kulisimamia vema taifa.

Magiri amesisitiza kuwa ushirika hauwezi kuendelea pasipo kuimarisha kilimo, na kwamba mchango wa MBIFACU katika kuongeza pato la taifa ni wa kupongezwa.

Akitilia mkazo umuhimu wa uongozi bora, Magiri amekumbusha kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi wa viongozi wa ushirika, hivyo amewataka wanachama kuchagua viongozi waadilifu na wenye maono.

Amesema ushirika ni chombo cha maendeleo na kinapaswa kusimamiwa kwa uaminifu na uwazi.

Viongozi waliopo na watakaochaguliwa wamehimizwa kusimamia fedha na rasilimali kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya kuhujumu uchumi au kuwanyanyasa wakulima.

Kwa upande wa maendeleo ya wakulima, Magiri ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwezesha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, hivyo akawaasa viongozi na wanachama kutomuangusha Rais.

Ameipongeza MBIFACU kwa hatua ya kujisajili kama kampuni na kujiendesha kwa mafanikio, huku akisisitiza kuwa ushirika si mali ya mtu binafsi bali ni mali ya wanachama wote, na kwamba lazima washiriki kikamilifu katika biashara kupitia kampuni yao.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya ushirika vilivyoko chini ya MBIFACU, Julius Mbunda ametoa ombi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuendeleza mpango wa ugawaji wa pembejeo kwa wakulima kwa njia endelevu.

Ameeleza kuwa hali ya maisha ya wakulima inaendelea kuimarika na mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano kati ya serikali na vyama vya ushirika.

Amewataka viongozi wa Amcos kuwa na uzalendo wa kweli, kuwa waaminifu na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa haki na kwa wakati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com