Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TARURA TUNDURU YAZINDUA BARABARA MPYA KWA KIWANGO CHA LAMI KUPITIA MBIO ZA MWENGE

Mwenge wa uhuru ulipofika katika eneo la kuzindua mradi wa barabara Nguzo sita-Muungano na Camp David Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Barabara yenye urefu wa kilometa 0.5 iliyozinduliwa na mbio za mwenge na kiongozi wa mbio hizo Ismail Ussi Wilayani Tunduru
Mhandisi Silvanus Ngonyani Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania Tarura Wilaya ya Tunduru akimuonyesha kiongozi wa mbio za mwenge Ismail Ussi kabla ya kuzindua mradi huo na kuweka jiwe la msingi.

Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, imezindua rasmi barabara mpya ya Nguzo Sita – Muungano – Camp David kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru, katika hafla iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

Uzinduzi huo umeashiria dhamira ya serikali kuboresha miundombinu ya barabara kwa maendeleo ya wananchi wa maeneo ya vijijini na Mijini.

Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Silvanus Ngonyani amesema kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 0.5 imejengwa kwa kiwango cha lami na ujenzi wake ulianza tarehe 28 Desemba 2023, ukitarajiwa kukamilika tarehe 15 Oktoba 2024 kwa mujibu wa mkataba.

Utekelezaji wa mradi huo umefanywa na mkandarasi M/S BR AND ASSOCIATES CONTRACTORS LIMITED kutoka Songea kwa gharama ya shilingi 234,902,000.00.

Mhandisi Ngonyani ameeleza kuwa kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na kuondoa udongo usiofaa (cut to spoil), kusawazisha kitako cha barabara (road bed), kuweka tabaka la kwanza la kifusi lenye unene wa sentimita 15 (G25), kufuatiwa na tabaka la pili la kifusi kilichochanganywa na saruji (CI) lenye unene huo huo, na kuweka tabaka mbili za lami pamoja na kokoto (double surface dressing).

Aidha, mradi umehusisha ujenzi wa makaravati manne, mitaro ya kupitisha maji, pamoja na ufungaji wa taa sita za barabarani kwa ajili ya mwanga usiku.

Mradi huo unatarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa cha usafiri na usafirishaji ndani ya eneo hilo, pamoja na kuinua shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Tunduru.

Mwenge wa Uhuru umetoa baraka na kuridhia ubora wa utekelezaji wa mradi huo, hatua inayodhihirisha azma ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia maendeleo ya miundombinu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com