Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Saimon Chacha akizungumza wakati mwenge wa uhuru ukiwa kwenye mradi wa maji uliopo katika kijiji cha Masuguru kabla ya kuwekwa kwa jiwe la msingi
Mradi wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA)Wilayani Tunduru ambapo kiongozi wa mbio za mwenge ameweka jiwe la msingi katika kijiji cha Masuguru Mradi huo ulipo
Na Regina Ndumbaro Masuguru-Tunduru
Mradi mkubwa wa maji safi na usafi wa mazingira unaotekelezwa katika kata ya Mchoteka, wilayani Tunduru kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 2,416,574,071.52.
Mradi huo utakapokamilika, unatarajiwa kuhudumia jumla ya wananchi 16,000, na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 81 hadi 86, sawa na ongezeko la asilimia 4.67.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Maua Mgaya amesema kuwa mradi huo utahudumia vijiji vinane vilivyopo katika kata ya Mchoteka, huku kazi ya ujenzi kwa sasa ikianza katika vijiji vya Mnemasi na Mchekeni.
Aidha, mradi huo tayari umewekwa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru kama ishara ya kukaguliwa na kuridhia ubora wa utekelezaji wake.
Mkazi wa kijiji cha Masuguru, Mariamu Said Rashid, ameonesha furaha yake kwa ujio wa mradi huo na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea huduma hiyo muhimu.
Amesema kuwa hapo awali walikumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi, hasa wakati wa masika walipotumia maji ya visima ambayo yalikuwa machafu na hatarishi kwa afya.
Ameomba mradi huo uwe endelevu na kuwaomba wahusika kuendelea na juhudi hizo.
Naye Ally Kaposa, mkazi mwingine wa kijiji cha Masuguru, amesema kuwa mradi huo umepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi, hasa kwa kuwa umewapunguzia wanawake adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Amesema kuwa tatizo hilo limesababisha migogoro ya ndoa kutokana na wanawake kuchelewa kurudi nyumbani.
Sasa, kwa upatikanaji wa maji karibu na makazi, wananchi wanaweza kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
Kaposa amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake ya "kumtua mama ndoo kichwani",
amesema kuwa kwao imefanikiwa kwa asilimia mia moja.
Amesisitiza kuwa wananchi wa Masuguru wanaendelea kumuombea heri Rais na kuahidi kushirikiana na serikali katika kutunza miundombinu ya mradi huo muhimu.
Social Plugin