Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA WILAYA YA MASASI AHAMASISHA WANANCHI KUJITOKEZA KUPOKEA MWENGE WA UHURU

 

Na Regina Ndumbaro-Masasi

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Rachel Kasanda, ametoa wito kwa wananchi wa Masasi kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru utakaowasili wilayani humo Mei 18, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mh. Rachel amesema Mwenge wa Uhuru ni alama ya umoja, amani na maendeleo, hivyo kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika mapokezi hayo muhimu kwa taifa.

 Rachel ameeleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha ulinzi na usalama wa kutosha wakati wa shughuli za mwenge, na kuwahakikishia wananchi kuwa mazingira yote yatakuwa salama. 

Amesisitiza kuwa ni fursa ya kipekee kwa wakazi wa Masasi kushuhudia uzinduzi na ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa ratiba, Mwenge wa Uhuru utakaa wilayani Masasi kwa siku mbili, ambapo Mei 18, 2025 utazindua miradi katika Halmashauri ya Mji wa Masasi, ukitokea Wilaya ya Nanyumbu. 

Siku inayofuata, Mei 19, Mwenge utaendelea na shughuli zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, hususan katika eneo la Mbuyuni.

Mwenge wa Uhuru utakamilisha mbio zake katika Wilaya ya Masasi kwa kukabidhiwa rasmi kwa Wilaya ya Newala tarehe 20 Mei 2025. 

Rachel amewahimiza wananchi kuonyesha mshikamano na uzalendo kwa kushiriki kwa amani na nidhamu katika shughuli zote zitakazoambatana na mbio hizo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com