Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngolo Malenya akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Saimon Chacha leo katika kijiji cha Mchoteka Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Ismail Ussi akiwaaga viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma baada ya Mwenge huo kupokelewa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Na Regina Ndumbaro Mchoteka-Tunduru
Mwenge wa Uhuru umeendelea na mbio zake katika kijiji cha Mchoteka kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, baada ya hafla ya makabidhiano rasmi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Saimon Chacha.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 15mwezi wa 2025 kwa heshima kubwa na ushiriki wa viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi.
Akizungumza mara baada ya kupokea Mwenge huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Saimon Chacha, amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa zaidi ya kilomita 100 katika wilaya hiyo.
Aidha, ameeleza kuwa mwenge huo utapitia kwenye maeneo mbalimbali ambapo utazindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Amesema miradi hiyo inaonyesha jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi kuleta maendeleo kwa wananchi wake kupitia utekelezaji wa miradi muhimu.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kwa mapokezi mazuri na kwa namna walivyoonesha heshima na upendo mkubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema kuwa usimamizi mzuri wa miradi ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Ismail Ussi ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu kinacholeta matumaini, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa mujibu wa Katiba kwa kwenda kupiga kura kwa amani na utulivu.
Amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, akisema kuwa kura ni silaha ya kuleta mabadiliko chanya.
Amewashukuru viongozi wa chama kwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali katika kuratibu mbio za Mwenge wa Uhuru.
Ushirikiano huo umeleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa shughuli za kitaifa kama hii, na ni ishara ya mshikamano unaojenga taifa lenye umoja na maendeleo.
Social Plugin