
Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, ameipongeza Kampeni ya Mama Samia Legal Aid kwa mchango wake mkubwa katika kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Ametoa pongezi hizo wakati akichangia mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, akibainisha kuwa kampeni hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wote wanapata haki kwa wakati, kwa karibu, na kwa usawa.
Mheshimiwa Mhagama amesema kuwa juhudi hizo za msaada wa kisheria zimeenda sambamba na ujenzi wa miundombinu ya mahakama nchini kote, jambo linaloimarisha upatikanaji wa haki hasa kwa wananchi waishio vijijini.
Ameeleza kuwa msaada huo si tu unaleta huduma za kisheria karibu na wananchi, bali pia unachochea amani na utulivu kwa kuwa haki ni msingi wa amani ya kweli katika jamii.
Ameongeza kuwa kampeni hii ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwahudumia Watanzania kwa usawa na haki bila kujali mahali walipo.
Amehimiza kuwa jitihada hizi zinaongeza imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria na utawala bora wa haki nchini.
Kutokana na mafanikio hayo, Mheshimiwa Mhagama amelihimiza Bunge Tukufu kuungana na Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria katika kuwapongeza viongozi wote walio mstari wa mbele katika utekelezaji wa kampeni hii.
Amewataja Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria; Mheshimiwa Jumanne Sagini, Naibu Waziri; Hamza Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali; na Eliakimu Maswi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na watendaji wote walio chini yao, kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa maslahi ya wananchi.
Social Plugin