Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADIWANI KILWA WAJADILI TAARIFA ZA UTEKELEZAJI




Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Bi Farida Kikoleka akizungumza na waheshimiwa Madiwani ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii FDC Wilayani Kilwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi Ndug Hemed Magaro akizungumza na waheshimiwa Madiwani katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii FDC

Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa limefanya mkutano tarehe 30 Aprili 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) Kilwa kwa ajili ya kujadili taarifa za utekelezaji wa kamati za kudumu za halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 (Januari hadi Machi 2025).

Aidha, mkutano huo umejadili pia taarifa za utekelezaji wa kamati za maendeleo ya kata kwa kipindi hicho hicho.

Katika kikao hicho, madiwani wamepata fursa ya kupitia na kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati husika.

Lengo kuu la mjadala huo ni kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia mipango na mikakati madhubuti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhe. Farida Kikoleka, ametoa wito kwa viongozi na wataalamu wa halmashauri kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unazingatia mahitaji halisi na vipaumbele vya wananchi.

Amehimiza miradi hiyo kutekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaokubalika ili kuleta tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Ndg. Hemed Magaro, amewataka madiwani kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo ni hatua muhimu ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu ni muhimu kwa mafanikio ya halmashauri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com