Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KITUO CHA AFYA TINGI SASA KUWA NA HUDUMA YA MAJI YA UHAKIKA


Kisima cha maji kilichosimamiwa na Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Tingi ambacho maji yake husukumwa kwa njia ya mota na kusaidia katika shughuli za kituo cha afya cha Tingi Mkoani Lindi
Baadhi ya viongozi na wananchi wa Kata ya Tingi Mkoani Lindi wakiwa eneo la kituo cha afya cha Tingi wakiangalia kisima hicho kilichochimbwa kwa nguvu ya usimamizi wa Diwani wa kata hiyo mheshimiwa Rajabu Ngatanda
Na Regina Ndumbaro Tingi-Lindi

Kituo cha Afya cha Tingi kilichopo katika kata ya Tingi, mkoani Lindi, sasa kina huduma ya maji ya uhakika kufuatia juhudi za diwani wa kata hiyo, Ndugu Rajabu Ngatanda. 

Uongozi wa kata hiyo umempongeza kwa jitihada zake ambazo zimeleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho muhimu.

Mganga mfawidhi wa kituo hicho, Bw. Jordan Maliga, ameeleza kuwa diwani huyo amehakikisha kuchimbwa kwa kisima na kuwekwa kwa mota ya kusukuma maji, hatua iliyosaidia kituo hicho kuwa na chanzo mbadala cha maji. 

Amebainisha kuwa hata maji kutoka Ruwasa yakikatika, huduma hazisimami kwa kuwa mota hiyo huwasaidia kuvuta maji kutoka kisimani kwa ufanisi.

Mwenyekiti wa UWT kata ya Tingi, Bi. Zuhura Mbungu, ameonesha furaha yake kwa hatua hizo, akisema kuwa juhudi za Mheshimiwa Diwani ni za kipekee na zinaonyesha kujitolea kwa dhati kwa ajili ya ustawi wa jamii. 

Ameongeza kuwa hayo ni muendelezo mzuri wa juhudi zake kwani hapo awali ameshatoa mabeseni na vifaa vya kujifungulia kwa ajili ya akina mama wajawazito.

Bi. Zuhura ameuomba uongozi wa afya katika wilaya na mkoa kuhakikisha wanaongeza idadi ya wataalam katika kituo hicho, kwani waliopo kwasasa hawatoshi na husababisha ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi. 

Amesisitiza kuwa uwepo wa maji pekee hautoshi bila rasilimali watu ya kutosha.

Kituo cha Afya Tingi kinahudumia pia kata jirani za Mingumbi, Miteja, Kinjumbi, na zamani Somanga, hali inayokifanya kuwa na mzigo mkubwa wa wagonjwa, hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu na maboresho ya miundombinu pamoja na rasilimali watu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com