Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANACHAMA 158 WAJIONDOA CHADEMA TANGA

Na Hadija Bagasha  - Tanga

Wanachama 158 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoani Tanga wamejiondoa kwenye chama hicho kwa madai kwamba chama hicho kimepoteza muelekeo na hivi sasa kimekuwa chama cha matusi,  kudharauliana na kukejeliana kwenye mitandao ya kijamii. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga Mjumbe wa Kamati ya mafunzo kanda ya Kaskazini Zainab Ashraf amesema kwamba wanaondoka katika chama hicho si kwamba wanamfuata aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe bali  sababu zilizowafanya wajiondoe ni kutokana na kupoteza muelekeo wa chama hicho pamoja na kukosekana kwa demokrasia ya kweli. 

"Tunajivua rasmi uanachama wa Chadema tutatafuta jukwaa jingine kwasababu wengi wetu hapa ni wanasiasa bado tuna ndoto zetu za kisiasa hazijatimia tutapata jukwaa jengine ambalo tutaliona ni rafiki na sisi kuendeleza harakati hizi za kutafuta demokrasia ya kweli na mapambano ya kweli kuwaokoa watanzania katika jukwaa tutakaloliona ni rafiki, "alisisitiza Zainabu

Aidha ameanisha sababu nyingine  kadhaa zilizowafanya kujiondoa kwenye chama hicho ikiwemo kukosekana kwa vikao hivi sasa lakini pia kimekuwa ni chama cha kutoa matamko kwenye majukwaa pamoja na kwenye mitandao ya kijamii huku wanaohoji masuala ya kichama wakiitwa Wahaini, wakitukanwa na kufukuzwa. 

"Kama chama chetu leo watu wakihoji wanaitwa Wahaini na hatukuwa na hayo mambo hiyo ni moja ya sababu tuone kwamba chama chetu sasa hakiamini katika demokrasia kinaamini katika udikteta kwamba usiulize wala usihoji lakini pia sababu nyingine ambayo tulikubalina hapa tujivue uanachama wa Chadema ni kuona chama chetu kimepoteza muelekeo, "alisema Zainabu. 

"Kwa hiki kinachoendelea Chadema hivi sasa kimekuwa ni chama cha majukwaa na kutoa matamko kwenye Social media hii ni moja ya sababu tukasema hapa hakuna tena chama tunaelekea kuwa ni NGO'S,"alisisitiza Mjumbe huyo. 

Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa baraza la vijana Jimbo la Tanga Hashim Jumanne amesema kwamba chama chao kimepoteza nidhamu hivyo walipofikia ni bora wastaafu siasa hizo na kubainisha kwamba hawamfuati mtu yeyote na badala yake wameamua wajivue uanachama wa Chadema ambapo wakati utakapofika kama kuna haja ya kuendelea na mapambano watatafuta jukwaa jingine la kuendeleza mapambano yao ya kisiasa. 

"Ukihitaji kwenye magroup yetu ya Chadema ma kwenye vikao upate kusifiwa wewe uwatukane viongozi ndio unaonekana kamanda na mpambanaji zaidi kila ambaye atamkashifu kiongozi na kumtolea maneno ya kejeli huyo ndio anaonekana kamanda na mpambanaji leo chama chetu anachokiandika Maria Sarungi na sio sio mwanachama wetu ni bora zaidi kuliko tunachokiandika sisi, "alisema  Jumanne. 

Naye Fatuma Mahinde Hamza aliyekuwa Katibu wa Wazee Mkoa wa Tanga kwa tiketi ya chama hicho amesema kwamba wamekuwa wakitafsiriwa tofauti kwamba wao wanaohama wanahama kwa kufuata vyeo jambo ambalo si kweli. 

""Kutokana na mwenendo mbovu wa chama chetu leo hii tumekaa sisi kama viongozi tukatafakari tuchukue hatua na hatua tuliyoichukua ni hii ya kjivua uanachama na tutakaa tukiangalia jukwaa la kwenda ili tukaendeleze mapambano kwakuwa bado tunalo jukumu na dhima ya kuwatetea watu wa Tanga, "amebainisha Fatuma. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com