Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kanali Patrik Sawala akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka katika Mkoa wa Ruvuma baada ya kuhitimisha ziara yake Mkoani humo
Kiongozi wa mbio za Mwenge Ismail Ussi akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrik Sawala na Watumishi wengine wa Mkoa huo
Na Regina Ndumbaro - Lumesule Mtwara
Mwenge wa Uhuru 2025 umepokelewa rasmi Mkoani Mtwara katika kijiji cha Lumesule ukitokea Mkoa wa Ruvuma.
Mapokezi hayo yameongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, huku wakazi wa Mtwara wakijitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Katika mkoa wa Mtwara, mwenge wa uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 974.5 kupitia halmashauri tisa.
Katika mbio hizo, mwenge utazindua, utakagua na kuweka mawe ya msingi kwenye jumla ya miradi 57 yenye thamani ya shilingi bilioni 18, ikiwemo miradi ya maendeleo ya jamii, afya, elimu, maji na miundombinu.
Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru zimeanza rasmi Mtwara leo tarehe 17 Mei 2025 na zitahitimishwa tarehe 25 Mei 2025.
Katika kipindi hicho, mwenge utapita kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuhamasisha maendeleo, mshikamano wa kitaifa na mapambano dhidi ya rushwa, UKIMWI na dawa za kulevya.
Baada ya kumaliza mbio zake mkoani Mtwara, mwenge wa uhuru utakabidhiwa kwa uongozi wa mkoa wa Lindi kwa ajili ya kuendelea na mbio zake katika mikoa mingine ya Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhimiza maendeleo na uzalendo miongoni mwa Watanzania.
Social Plugin