Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFUGAJI WA KUKU RUVUMA WAPATIWA MAFUNZO YA UFUGAJI BORA



Daktari wa Wanyama wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Dkt. Seria Masole akiwaonyesha wafugaji katika mafunzo ya namna bora ya ufugaji wa kuku na aina za Dawa ya kuku zinazotakiwa kutumika
Daktari wa Wanyama wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Dkt. Seria Masole akiwaonyesha wafugaji katika mafunzo ya namna bora ya ufugaji wa kuku na aina za Dawa ya kuku zinazotakiwa kutumika
Dkt. Julius Gerase Prosper kutoka kampuni ya ASHISHI LIFE SCIENCE LTD akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo na namna ya kutunza mifugo hiyo ya kuku


Picha ya pamoja ya wafugaji walioshiriki semina hiyo na mtoa semina wa mafunzo hayo Dkt. Julius Gerase kutoka Shirika la ASHISHI LIFE SCIENCE LTD Dkt. Seria Masole kutoka Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Wafugaji wa kuku kutoka manispaa ya Songea, Mkoani Ruvuma, wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu ya ufugaji bora wa kuku katika semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa Songea Girls.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuongeza uelewa wa wafugaji kuhusu mbinu sahihi za ufugaji zenye tija na zenye kuzingatia afya na ustawi wa mifugo.

Akizungumza katika semina hiyo, Daktari wa Mifugo wa Manispaa ya Songea, Dkt. Seria Masole, ameeleza kuwa elimu ya ufugaji ni msingi muhimu katika kuendeleza sekta ya mifugo nchini.

Amebainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wafugaji wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mbinu sahihi za ufugaji, hali inayosababisha uzalishaji usioridhisha na hasara kwa wafugaji.

Amesisitiza kuwa mafunzo kama haya yanatoa fursa kwa wafugaji kujifunza kwa vitendo kuhusu lishe bora ya kuku, matumizi sahihi ya dawa na chanjo, pamoja na mbinu za kuboresha mazingira ya kufugia.

“Ni muhimu kwa kila mfugaji kutambua kuwa mafanikio ya ufugaji hayategemei tu kuwa na kuku wengi, bali ni kufuga kwa kuzingatia kanuni bora, afya ya mifugo, na usafi wa mazingira,”ameeleza Dkt. Masole.

Ameongeza kuwa lengo lake ni kuhakikisha wafugaji wote wanapata elimu ya msingi itakayowawezesha kuongeza tija, kipato na kuboresha maisha yao.

Mtaalamu aliyetoa mafunzo hayo, Dkt. Julius Gerase Prosper kutoka kampuni ya ASHISHI LIFE SCIENCE LTD, amesema kuwa lengo la mafunzo ni kuhakikisha kuwa wafugaji wanafanya ufugaji wa kitaalamu kwa manufaa yao binafsi na jamii kwa ujumla.

Ameeleza kuwa mfugaji anatakiwa anufaike na kile anachokifanya kwa kufuata kanuni bora za ufugaji.

Dkt. Julius amebainisha mambo muhimu yanayoathiri ufugaji wa kuku ikiwa ni pamoja na afya ya kuku, usafi wa vyombo vya chakula na maji, na matumizi sahihi ya dawa na chanjo.

Ameelekeza kuwa ni muhimu kuhakikisha chakula cha kuku kinamalizika kabla ya kuongeza kingine ili kuepuka uchafuzi wa mazingira na magonjwa.

Aidha, amehimiza wafugaji kutozidisha matumizi ya dawa bila mpangilio na kuelewa muda sahihi wa kutoa virutubisho

Kwa upande wao, baadhi ya wafugaji walioshiriki semina hiyo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata huku wakiahidi kuitumia ipasavyo katika shughuli zao za kila siku.

Wamesema kuwa wamejifunza mbinu mpya ambazo hawakuwahi kufahamu awali na sasa wako tayari kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa wafugaji wengine.

Semina hiyo imeleta matumaini mapya kwa wafugaji wa kuku katika mkoa wa Ruvuma, ambao sasa wanatarajia kuongeza tija katika ufugaji wao na kuchangia katika uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Dkt. Julius Gerase Prosper kutoka kampuni ya ASHISHI LIFE SCIENCE LTD akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo na namna ya kutunza mifugo hiyo ya kuku

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com