Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGAWANYIKO WAZUKA KWA MADIWANI WA MSALALA SAKATA LA MBUNGE IDD KASSIM KUJADILIWA KWENYE KIKAO

Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog

Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, kimeibua mvutano mkali baada ya baadhi ya madiwani kupinga hatua ya kumjadili Mbunge wa Jimbo hilo, Iddi Kassim, wakidai kuwa kikao hicho kilikiuka taratibu na miongozo ya uendeshaji wa vikao vya kisheria.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo, Baadhi ya madiwani wamepinga vikali pendekezo la kumfikisha Mbunge huyo mbele ya Kamati ya Maadili ya Madiwani, wakimtuhumu kwa kuwadhalilisha kwenye mikutano ya hadhara katika maeneo yao ya uwakilishi. Hoja hiyo iliibuliwa kwenye kikao cha Aprili 30 mwaka huu, ambapo baadhi ya madiwani waliunga mkono hatua hiyo wakidai Mbunge amekuwa akiwahoji hadharani bila utaratibu.

Hoja hiyo iliwasilishwa na Diwani wa Segese, Joseph Manyala, na kuungwa mkono na madiwani wengine akiwemo Shija Luyombya (Bulyanhulu), Samson Masanja (Mwanase), na Nyagwema Mnyirwa (Viti Maalumu – Bulyanhulu).

Hata hivyo, Diwani wa Busangi, Alexander Mihayo, amepinga hatua hiyo akisema haikufikiwa kwa makubaliano ya pamoja.

Amesisitiza kuwa kikao hicho kiliongozwa bila kufuata kanuni, kwani ajenda ya kumjadili Mbunge haikuwamo kwenye ratiba rasmi ya kikao.

Ameongeza kuwa baadhi ya madiwani wanaomuunga mkono Mbunge wanamuona kama anahamasisha uwajibikaji kwa kuwa huwaweka mbele kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi – jambo ambalo halipaswi kuchukuliwa kama dharau.

“Tunapoelekea uchaguzi mkuu, ni wajibu wetu kuwa na majibu mbele ya wananchi. Mbunge anaposimamisha diwani kueleza maendeleo ya kata yake, si dharau bali ni kuwajibika kwa wananchi,” amesema Mihayo.

Pily Izengo, Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Isaka, amesema ameshiriki ziara nyingi na Mbunge huyo na hajawahi kushuhudia diwani yeyote akidhalilishwa.

Ameongeza kuwa ndani ya mfuko wa jimbo, fedha hugawiwa kwa kuzingatia mahitaji ya kila kata na hadi sasa zaidi ya Shilingi milioni 79 zimeshatolewa kusaidia miradi yenye changamoto kubwa.

Kwa upande wake, Diwani wa Ngaya, Kisusi Ilindilo, amesema kuwa Mbunge Kassimu alisaidia sana kufanikisha upatikanaji wa umeme katika kata yao, ikiwa ni pamoja na vijiji na vitongoji vyote pamoja na kituo cha afya, hali iliyorahisisha huduma kwa wajawazito.

Naye Frola Sagasaga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa Mwalungulu, ameeleza kuwa kikao cha Aprili 30 hakikufuata utaratibu wa upatikanaji wa ajenda, kwani kwa mujibu wa taratibu, hoja kama hiyo inapaswa kuanza kujadiliwa kwenye kikao cha chama (Kokasi) kabla ya kufikishwa kwenye baraza la madiwani.

Amebainisha kuwa hata yeye aliwahi kuulizwa na wananchi kuhusu miradi ya maendeleo kwenye mkutano wa hadhara, lakini kwa kuwa alikuwa na majibu sahihi, hakupata ugumu kueleza hatua za utekelezaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com