Mwenyekiti Wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Hairu Hemed Mussa akizungumza wakati wa kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Chiza Cypirian Marando akitoa ufafanuzi wa swali la mheshimiwa Diwani wa Kata ya Chiwana Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Na Regina Ndumbaro -Ruvuma.
Kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kimefanyika tarehe 11 Aprili 2025 kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Hairu Hemed Mussa, ambaye ameeleza kuwa Halmashauri imeendelea kutekeleza majukumu muhimu kama vile ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na mshikamano mzuri kati ya madiwani, uongozi wa chama na serikali.
Katika kipindi hicho, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imekusanya jumla ya shilingi bilioni 6.896 milioni 620,261.63, sawa na asilimia 123.10 ya makisio yake ya mapato ya ndani.
Mwenyekiti Mussa amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mashine za POS katika ngazi ya vijiji na kata pamoja na hatua za kudhibiti mapato yaliyokuwa yakitoroshwa.
Ameeleza kuwa Halmashauri itaendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha.
Katika sekta ya elimu, Halmashauri imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa shule mpya za sekondari ikiwemo Namakambare, Mbati – Mtina, pamoja na maandalizi ya miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule za Mataka, Nakapanya, Matemanga, Mchoteka na Masonya.
Aidha, kupitia programu ya BOOST, miradi mbalimbali ya ujenzi katika shule za msingi ipo katika hatua ya utekelezaji kwa asilimia 75.
Katika sekta ya afya, elimu na maji, miundombinu imeboreshwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Halmashauri pia imefanikiwa kugawa fedha kwa wanufaika wa kaya maskini katika vijiji vyote 157, ambapo kaya 12,015 zimenufaika na mpango huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri amewataka madiwani kuendeleza mshikamano ili kuimarisha maendeleo katika wilaya hiyo, huku akitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu kama afya, elimu, barabara, umeme, maji na mawasiliano kwa karibu.
Katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Chiwana Rashidi Sued Makunganya ameuliza swali kuhusu uwepo wa ofisi ya Chama cha Ushirika katika kata yake, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Chiza Cypirian Marando, amejibu kuwa maombi hayo yamepokelewa na yatawasilishwa kwa viongozi husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Madiwani wameipongeza Idara ya Elimu kwa kazi nzuri na kusisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha mafanikio endelevu katika Halmashauri yao.
Social Plugin