

Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma.
Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) limeleta huduma zake Wilayani Tunduru, Mkoani Ruvuma, kwa lengo la kusogeza huduma za bima ya afya karibu na wananchi wa eneo hilo.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Ruvuma, Hans John, ametoa taarifa hiyo leo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha huduma za afya bora na nafuu zinawafikia Watanzania wote bila kujali hali zao za kiuchumi.
Hans John ameeleza kuwa kwa sasa takriban Watanzania milioni 45 bado hawajajiunga na huduma ya bima ya afya, jambo linalohitaji juhudi kubwa za uelimishaji kwa jamii.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa faida za kuwa na bima ya afya, akibainisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza muswada wa kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima hiyo.
Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari amesaini sheria ya kuimarisha huduma hiyo na kuifanya ipatikane kwa makundi yote ya jamii.
Awali, huduma ya NHIF ilihusisha zaidi wafanyakazi wa serikali pekee, lakini sasa imepanuka na kuwajumuisha watumishi wa sekta binafsi, wanafunzi, na wananchi wa kawaida.
Meneja huyo ameeleza kuwa hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za afya kwa urahisi.
Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wa ngazi mbalimbali wana wajibu wa kuhamasisha wananchi wao kujiunga na mfuko huo ili waweze kunufaika na matibabu katika hospitali za wilaya, mkoa, na kanda.
Vilevile, Hans John ameeleza kuwa NHIF ina vifurushi viwili vinavyotoa huduma tofauti, ambavyo ni kifurushi cha Ngorongoro na cha Serengeti, vyote vikisimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima.
Ameongeza kuwa mfuko huo pia umeanzisha utaratibu wa kuwatambua wananchi wasio na uwezo wa kujiunga na bima kwa gharama zao, ili waweze kusaidiwa na serikali.
Pia, ameeleza kuwa huduma zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa, ambapo sasa madai yote ya wanachama yanaingizwa kwenye mfumo wa kidigitali na wanachama wanaweza kufuatilia taarifa zao kwa urahisi.
Meneja huyo ametoa wito kwa viongozi na waandishi wa habari kushirikiana kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuwa na bima ya afya, hasa kwa watoto.
Amesema serikali inataka kuona kila mtoto nchini anapata huduma ya afya kupitia bima, jambo litakalosaidia kulinda afya ya vizazi vijavyo na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia nyingi.
Amesema NHIF iko tayari kushirikiana na wadau wote katika utekelezaji wa mpango huu kwa mafanikio makubwa.
Social Plugin