
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera
Na Lydia Lugakila - Kyerwa
Wataalam wa Afya Wilayani Kyerwa Mkoani Kagera wametakiwa kuwafuatilia watoto 15 waliyoonyesha dalili za ugonjwa wa surua Lubella unaotajwa kujitokeza Wilayani humo.
Agizo hilo limekuja kufuatia kusomwa kwa andiko lililohusu uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa surua Lubella katika kijiji cha Kyerwa kata ya Kyerwa lililosomwa na Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa Gordian Rugaimukamu kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ikiwa ni maelekezo ya Serikali.
Akizungumzia mlipuko wa ugonjwa wa Surua Lubella Rugaimukamu amesema kuwa ugonjwa huo umethibitika Februari 22,2025 baada ya sampuli 5 za wahisiwa kuchukuliwa na majibu ya sampuli 4 kukutwa na maambukizi ya virusi vya surua ambapo timu ya wataalam wa Afya ngazi ya Halmashauri imeanza kampeni ndogo ya utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo mnamo Februari 24,2025 itakayohusisha watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miaka 5 huku watoto 15 wakifuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha wanapata tiba na kuzuia maambukizi.
Amesema lengo la kampeni hiyo ni kuzuia ugonjwa huo usisambae ambapo tangu kampeni hiyo kuanza jumla ya watoto 9,88 wamepata chanjo ya kuwakinga dhidi ya surua Lubella.
Rugaimukamu ameongeza kuwa ugonjwa wa Surua ni ugonjwa unaoathiri watu wa rika zote ambapo watoto chini ya miaka mitano huathirika zaidi.
"Ugonjwa huo uenea kwa njia ya hewa hususan mgonjwa anapokohoa au kupiga ambapo maambukizi huwa ni ya haraka sana hasa sehemu zenye msongamano", amesema Rugaimukamu.
Ametaja dalili za ugonjwa huo amesema kuwa ni homa,mafua, kikohozi, macho kuwa mekundu na kutoa machozi, kutokwa na vipele vidogo vidogo ambavyo uanza kutoka kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima.
Aidha amesema madhara ya ugonjwa wa Surua Lubella ni makubwa kwani huweza kusababisha masikio kutoa usaha na kupelekwa matatizo ya kutokusikia, vidonda vya macho vinavyoweza kusababisha upofu wa macho, homa ya mapafu- nimonia, utapiamlo na kuwa endapo mgonjwa hatopata tiba sahihi kwa wakati anaweza kupata ulemavu au kupoteza maisha
"Ugonjwa huo unazuilika kwa chanjo mtoto atapata dozi 2 za chanjo ya kumkinga ambazo hutolewa mtoto anapofikisha umri wa miezi 9 na marudio ni pale mtoto anapofikisha wa miezi 18", amesema kiongozi huyo.
Amesema mtoto anaweza pia kupata dozi nyingine ya surua wakati wa kampeni za chanjo husika.
Ametoa wito kwa Wananchi kuwapeleka watoto kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo ili maambukizi yasiendelee katika eneo hilo.
Social Plugin