
Kanali Ahmed Abbas Ahmed, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akiongoza kikao ch baraza la Biashara ukumbi wa Manispaa Songea Mkoani Ruvuma

Baadhi ya Wafanyabiashara na Watumishi wa Serikali waliohudhuria katika baraza hilo ukumbi wa Manispaa Songea Mkoani Ruvuma

Katibu Tawala wa Mkoa Marry Makondo akizungumza na wafanyabiashara ukumbi wa Manispaa Songea Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro - Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameongoza kikao cha Baraza la Biashara cha Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta binafsi na Serikali kwa lengo la kujadili changamoto na fursa za biashara katika mkoa huo.
Akifungua kikao hicho, Kanali Ahmed amewapongeza wafanyabiashara kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa Baraza la Biashara ni jukwaa muhimu la majadiliano kati ya sekta binafsi na Serikali, likilenga kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya biashara.
Mkuu wa Mkoa amewaagiza watendaji wa Serikali katika ngazi zote kuhakikisha vikao vya Baraza la Biashara vinafanyika kila mwaka kwa mujibu wa mwongozo.
Amesisitiza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi na itaendelea kushirikiana nao kuboresha mazingira ya biashara.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, ameeleza kuwa biashara ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha uchumi wa Mkoa wa Ruvuma unakua na kunufaisha wananchi wote.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Kudrack Darajani amewasilisha baadhi ya maombi ya wafanyabiashara kwa Serikali.
Miongoni mwa maombi hayo ni pamoja na VAT kutozwa viwandani na mipakani, kufutwa kwa faini zinazotokana na mashine za EFD, na kuwekwa uwazi katika makadirio ya mapato ili kuondoa mkanganyiko kwa wafanyabiashara.
Wafanyabiashara wametumia fursa hiyo kueleza changamoto wanazokumbana nazo, huku wakiiomba Serikali kuzifanyia kazi ili kuboresha mazingira ya biashara.
Pia wameeleza kuwa uboreshaji wa mifumo ya ushuru na utoaji wa leseni utawasaidia kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa maazimio mbalimbali yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara mkoani Ruvuma.
Serikali iliahidi kuyafanyia kazi maombi yaliyowasilishwa na kuhakikisha majadiliano kama hayo yanaendelea kufanyika kwa maendeleo ya uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Social Plugin