Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WAUMINI na Askari Magereza wa Gereza la Isanga wamemshukuru Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma Mustapha Rajabu kwa kutoa tofali 1000 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa wafungwa na mahabusu katika eneo la Isanga Magereza Jijini Dodoma.
Shukrani hizo wamezitoa Leo Machi 13,Jijini hapa wakati walipofika ofisini kwake katika msikiti wa Gaddafi kwa lengo la kumshukuru na kumpatia ramani ya ujenzi wa msikiti huo.
Akizungumza kwa niaba yao,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza (SACP) Makao Makuu,Daimu Mmolosha amesema wanamshukuru Sheike Rajabu kwa kuwasaidia tofali 1000 kwani kitendo hicho ni Cha kiungwana.
"Kwa niaba ya Waumini wa Magereza tunakushukuru kwa kutushika mkono,wafungwa na mahabusu bado wanachangamoto ya kuwa na eneo zuri kwa ajili ya kuabudu kwa hichi ulichofanya tunasema asante,"amesema Kamishna Msaidizi Mmolosha
Kamishna Msaidizi,Mmolosha amesema wanahitaji zaidi ya Sh milioni 83 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa msikiti huo wa kisasa ambao utawasaidia wafungwa,mahabusu na Askari kuweza kuabudu.
Kwa upande wake Sheike Rajabu amewashukuru Waumini hao kwa kuonesha utu kwa kumfuata ofsini kwake na kumshukuru.
"Nashukuru kwa wema wenu na nimefurahishwa kwa kuonesha wema wenu,mmetekeleza ile kauli asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi kushukuru,Kuna sehemu nyingi tunasaidia lakini hatushukuriwi,"amesema Sheikhe Rajabu.
Amesema kwa kushirikiana na wadau na marafiki zake atahakikisha msikiti huo unajengwa na unakamilika mpaka ifikapo Ramadhan ijayo.
"Ninahistoria na ule msikiti,nimewahi kuwa mwalimu wa Madrasa miaka hiyo,ilivyokuwa miaka hiyo ndivyo ulivyo Sasa,,jambo hili siwezi kukubali hapa ni Makao Makuu lazima majengo yaendane na hadhi ya Makao Makuu,"amesema Sheikhe Rajabu.
Social Plugin