Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA RUVUMA ODDO MWISHO ATEMBELEA SHULE YA MSINGI LUMALU KUTOA POLE

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho akiongea na walimu wa shule ya msingi Lumalu pamoja na wananchi
Wananchi waliojitokeza katika shule ya msingi Lumalu pamoja na walimu wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa Oddo Mwisho

Na Regina Ndumbaro - Nyasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, ametembelea Shule ya Msingi Lumalu iliyopo katika Kata ya Upolo, Wilaya ya Nyasa, kwa lengo la kutoa pole kwa walimu na wananchi wa kijiji cha Lumalu. 

Ziara hiyo imefanyika leo kufuatia msiba wa walimu wanne wa shule hiyo waliopoteza maisha katika ajali hivi karibuni.

Akizungumza na walimu na wananchi, Mwenyekiti Oddo Mwisho amewapa pole kwa msiba huo mzito na kueleza kuwa aliahidi kuitembelea shule hiyo ili kuwafariji walimu na wananchi wa eneo hilo. 


Aidha, Mwenyekiti huyo amewaomba wananchi wa Lumalu kushirikiana na walimu waliobaki badala ya kueneza dhana potofu kuhusu ajali hiyo. 

Amesisitiza kuwa badala ya kuzungumzia kwa namna hasi tukio hilo, jamii inapaswa kuwa na mshikamano, upendo, na kusaidiana ili kuhakikisha elimu inaendelea kuimarika katika kijiji hicho.

Katika hatua nyingine, Oddo Mwisho amebainisha kuwa upungufu wa walimu umeathiri kiwango cha ufaulu katika shule hiyo. 

Ameahidi kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Ofisi ya Utumishi ili kuhakikisha shule hiyo inapata walimu wa kutosha kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kushirikiana na walimu katika kuwahamasisha wanafunzi kujituma zaidi kwenye masomo yao. 

Amesema kuwa mafanikio ya shule hayawezi kupatikana bila ushirikiano kati ya jamii, walimu, na wanafunzi wenyewe.

Kwa upande wake, Mwalimu Nicholaus Mahundi wa Shule ya Msingi Lumalu amempongeza Mwenyekiti huyo kwa kuja kuwapa pole na faraja katika kipindi hiki kigumu. 

Aidha, ameiomba serikali kuboresha miundombinu ya madarasa pamoja na kuongeza walimu shuleni hapo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na wanafanya vizuri katika masomo yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com