Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJENZI WA BARABARA YA AMANIMAKOLO-RUANDA HADI BANDARI YA NDUMBI WAFIKIA ASILIMIA 40


Meneja mradi wa Ujenzi wa Barabara ya lami ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Ruvuma kutoka Kampuni ya China Railway Seventh Group(CRSG) GE Guanghua wa pili kushoto,akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) Mkoa wa Ruvu
Ujenzi wa Barabara ya lami ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma ukiendelea kama inavyoonekana.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Saleh Juma aliyeshika magoti,akiangalia vipimo vinavyoonesha ubora wa lami iliyowekwa kwenye wa barabara ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Mbinga hadi Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya lami ya Amanimakolo-Ruanda Wilaya ya Nyasa kuelekea Bandari ya Ndumbi Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma ikiwa ni sehemu ya Mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan



Na Regina Ndumbaro-Mbinga. 

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma umeanza ujenzi wa awamu ya pili wa barabara ya Amanimakolo-Ruanda hadi Bandari ya Ndumbi yenye urefu wa kilometa 95 kwa kiwango cha lami. 

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Saleh Juma, amesema ujenzi wa barabara hiyo unafanyika kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza iliyohusisha kipande cha Kitai hadi Amanimakolo chenye kilometa tano tayari imekamilika na inatumika.

Kwa sasa, mkandarasi yupo katika hatua za mwisho za kuweka tabaka la lami katika kipande cha kilometa mbili kati ya kilometa 35 za awamu ya pili zinazoanzia kijiji cha Amanimakolo hadi kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga. 

Meneja wa TANROADS ameongeza kuwa, baada ya kukamilika kwa sehemu hiyo, awamu ya tatu ya ujenzi itaanza kutoka kijiji cha Ruanda kupitia Lituhi hadi Bandari ya Ndumbi wilayani Nyasa, hatua ambayo itawezesha wananchi wa maeneo hayo kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.

Kwa mujibu wa Saleh Juma, mradi huo ni sehemu ya mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 Pia ameeleza kuwa ujenzi wa Bandari ya Ndumbi umekamilika kwa zaidi ya miaka miwili sasa, na kilichosalia ni kukamilika kwa barabara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Mkoa wa Ruvuma kwenda mikoa mingine na nchi jirani ya Malawi.

Mhandisi Anselem Chambila kutoka ofisi ya TANROADS Mkoa wa Ruvuma amesema kuwa kati ya kilometa 35 zinazojengwa katika awamu ya pili, tayari kilometa tano zimeanza kujengwa huku kilometa mbili zikiwa hatua ya mwisho za ukamilishaji. 

Amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri na kinachosubiriwa kwa sasa ni fedha kutoka Serikali ili kukamilisha kilometa zote 35 na kuruhusu wananchi kutumia barabara hiyo kwa shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wake, Meneja wa mradi huo kutoka Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG), GE Guanghua, amesema ujenzi umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake. 

Ameeleza kuwa kazi inaendelea kwa kasi ili kuhakikisha barabara inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Amanimakolo wameipongeza Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo, wakisema itakapokamilika itasaidia kurahisisha usafiri na kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo yao. 

Wamesema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa wananchi kwa kuwa itawasaidia kusafirisha bidhaa kama samaki na dagaa kutoka Ziwa Nyasa kwenda maeneo mengine kwa urahisi zaidi.

Hata hivyo, wananchi hao wameitaka TANROADS kuhakikisha inamsimamia mkandarasi kwa karibu ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati. 

Wamesema ujenzi wa barabara hiyo umekuwa ukichukua muda mrefu bila kukamilika, hivyo wanahitaji juhudi zaidi ili kazi hiyo iishe haraka na kuondoa changamoto za usafiri katika eneo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com