Na Mwandishi Wetu, KILIMANJARO
Mkuu wa Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, Dkt. Christopher Timbuka, amewataka watumishi waliopatiwa mafunzo ya utawala bora wilayani humo kutekeleza kwa vitendo maarifa hayo katika kushughulikia changamoto za wananchi, ili kuhakikisha utawala bora unaendelea kuimarika katika jamii.
Dkt. Timbuka ameyasema hayo leo, Februari 6, 2025, wakati akifungua mafunzo ya Uraia na Utawala Bora, yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utawala bora, haki za kiraia, na uwajibikaji wa viongozi kwa jamii.
"Serikali imejidhatiti kutoa mafunzo haya kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha kwamba wanakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwa mfano mzuri wa uongozi. Tunataka kuona vitendo bora vinavyoendana na maarifa haya," amesema Dkt. Timbuka.
Dkt. Timbuka amesisitiza umuhimu wa viongozi waliopokea mafunzo hayo kuyapeleka kwa vitendo yale waliyojifunza kwa kushirikiana na wananchi.
Amewasihi viongozi hao kuwahamasisha na kuelimisha wenzao ili kuwa na mtindo mmoja wa kiutendaji, hivyo kusaidia katika kuboresha utawala na huduma kwa jamii.
"Tubadilike kupitia haya mafunzo, elimu hii ikatatue shida za wananchi," amesema Dkt. Timbuka, akihimiza kuwa mafunzo haya si tu kwa manufaa ya viongozi, bali pia ni kwa faida ya jamii nzima.
Ameongeza kuwa, kupitia utekelezaji wa maarifa hayo, kero za wananchi zitaweza kutatuliwa kwa haraka na kwa ufanisi, na hivyo kuboresha hali ya maisha katika wilaya ya Siha.
Kwa upande wake Pilly Ali Abdalah, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Garagua, ameelezea manufaa ya mafunzo hayo, akisema kuwa yametia mkazo katika kuimarisha usalama na ulinzi katika kata na vijiji, jambo ambalo linachangia katika uimarishaji wa utawala bora katika ngazi ya chini.
Amesisitiza kuwa, wamepata uelewa wa kina kuhusu namna ya kushughulikia kero za wananchi na kuwaelimisha kuhusu haki zao, hivyo kuhakikisha usawa na haki kwa wote.
"Kwa ujumla, mafunzo haya yametujenga na kutufundisha wajibu wetu kama viongozi. Tumekumbushwa kwamba tunatakiwa tutende haki kwa jamii, kuepuka migogoro, na kuwa na uhusiano mzuri kati ya serikali na wananchi," amesema Abdalah.
Pamoja na hayo, Afisa huyo amesisitiza kuwa, katika utawala bora, suala la kutunza siri za wananchi ni muhimu ili kulinda maadili ya uongozi.
Ameweka wazi kuwa, utawala bora unahitaji viongozi kufanya kazi kwa bidii, kuwa waaminifu, na kujiepusha na vitendo vya kukiuka maadili ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Ameongeza kuwa, endapo viongozi watazingatia misingi ya utawala bora, migongano kati ya serikali na wananchi itaepukwa, na hivyo utawala bora utaweza kustawi.
"Kwa hiyo, ili tuwe na utawala bora, ni lazima tuzingatie misingi ya haki, uwazi, na uwajibikaji. Kazi yetu ni kuhakikisha kwamba tunaimarisha uhusiano mzuri kati ya serikali na wananchi, ili jamii iwe na amani na maendeleo," alisema Abdalah.
Mafunzo haya ya Uraia na Utawala Bora ni sehemu muhimu ya mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kuwa viongozi wa ngazi zote wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utawala bora, na wanatekeleza majukumu yao kwa uwazi na ufanisi, ili kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.
Social Plugin