Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA MBUZI 168 WAIBIWA MWAKA 2024 KATA KITOBO WILAYANI MISENYI


#Wananchi Waamua kulala na mifugo karibu na vitanda vyao

Na Lydia Lugakila - Misenyi

Baadhi ya Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi Mkoani Kagera wametoa taarifa juu ya uwepo wa wimbi la wizi wa mifugo uliosababisha hasara kwa Wananchi ambapo zaidi ya mbuzi 168 waliibiwa mwaka 2024 katika kata ya Kitobo huku katika kata ya Bugorora Wilayani humo mbuzi wakidaiwa kuchinjwa wakiwa zizini.

Hayo yamejiri baada Madiwani wa Halmashauri hiyo kutoa taarifa za kata  katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi kilichoketi februari 27,2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya kata ya kitobo Diwani wa kata hiyo mhe,Willy Mutayoba amesema ndani ya mwaka mzima wa 2024 kata yake imepata hasara kwani zaidi ya mbuzi 168 waliibiwa ndani ya vijiji vitano vya kata hiyo na kuleta hofu kubwa kwa Wananchi baada ya kupata hasara hiyo.

"Mbuzi 15 uibiwa kila
mwezi hiyo ni hasara kubwa kwa Wananchi na ndo maana Wananchi wanaamua kulala na mifugo yao karibu na vitanda vyao"amesema mhe, Mutayoba.

Mutayoba ameongeza kuwa wizi huo umeshamili katika kila kata japo yeye kapata kujua takwimu za haraka katika eneo lake lakini vilio vingi katika kata nyingine wizi wa mifugo umeendelea.

Amesema Wananchi wengi hutegemea kuinua vipato vyao kupitia kuuza mbuzi Ng'ombe, na mazao mengine hivyo wizi huo umewaletea hasara kubwa huku akiomba mpango wa haraka ufanyike ili kuwanusuru Wananchi hao dhidi ya wimbi hilo.

Aidha amesema kamati ya ulinzi na usalama iliyoko chini ya mtendaji wa kata wana taarifa juu ya matukio hayo ambapo walianzisha suala la ulinzi shirikishi licha ya hatua hiyo kutozaa matunda.

"Ulinzi shirikishi unafanyika leo kesho wanaiba hali hii inatisha lazima tupate muafaka wa haraka" amesema Willy.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bugorora Mhe, Renovatus Rumanyika amesema wizi wa mifugo midogo midogo hasa mbuzi upo katika vijiji vyote vya Wilaya hiyo ambapo wezi hao ufika na kuchinja mbuzi baada ya kuwaiba kutoka zizini na kuondoka na nyama huku utumbo ukiachwa maeneo ya mifugo hiyo.

Kufuatia hali wamuomba Mkuu wa Wilaya ya Misenyi kukomesha wizi huo kwa haraka ili Wananchi wawe na amani na mifugo yao.

Naye Diwani wa kata ya Kashenye ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi Domician Nshekanabo Nshambya amekiri kuwepo kwa wizi wa mifugo na kwamba wameelekeza suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya ili alifanyie kazi kwa ukaribu sana  na kuwaondolea Wananchi changamoto hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nkenge Mhe, Florent Kyombo amesema changamoto ya wizi wa mifugo imejirudia ambapo katika ziara aliyoifanya mwezi Novemba, 2024 katika mikutano yake Wananchi walilalamika juu suala hilo ambapo tayari lilishaanza kufanyiwa kazi baada ya kukabidhiwa kwenye kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mkuu wa Wilaya hiyo.

Kyombo ameahidi kuweka msisitizo kwa mhe, Mkuu wa Wilaya  ili ahakikishe analifanyia kazi kwa haraka na kulikomesha mara moja.

Hata hivyo mbunge Kyombo pamoja na Madiwani wa Halmashauri hiyo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu hassan kwa kuendelea kutekeleza ilani ya CCM na kuleta maendeleo kwa Wananchi na Watanzania kwa ujumla huku wakiahidi kumuunga mkono kwa kumpatia zawadi ya kura ili aendeleze juhudi za kuwaletea maendeleo Watanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com