
Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Bi Pendo Daniel akimkabidhi mjasiriamali Joyce Hyera wakati wa ugawaji wa vitambulisho hivyo
Na Regina Ndumbaro-Mbinga.
Wajasiriamali wadogo wa maeneo ya Kigonsera na Mkako, wilayani Mbinga, wamepokea vitambulisho maalum vya utambulisho kwa lengo la kuwawezesha kupata mikopo na kutambulika rasmi na serikali.
Ugawaji wa vitambulisho hivyo umefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, ambapo hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wajasiliamali wadogo wa eneo hilo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga, Pendo Daniel, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Kisare Batiku Makori.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Pendo Daniel amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inatambua mchango mkubwa wa wajasiriamali wadogo katika kukuza uchumi wa taifa.
Pia, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuanzisha programu hii inayolenga kuinua hali ya maisha ya wajasiliamali wadogo.
Aidha, ameeleza kuwa utoaji wa vitambulisho hivyo unalenga kuwasaidia wajasiriamali hao kujikwamua kiuchumi na kijamii, pamoja na kuwapatia fursa za kutambulika katika taasisi za kifedha, hasa Benki ya NMB.
Pia, ametoa wito kwa wakazi wa Kigonsera kuhakikisha wanapata vitambulisho hivyo na kwa wale ambao bado hawajasajili vikundi vya ujasiriamali kujisajili, kwani mpango huu ni endelevu na unatoa fursa ya upatikanaji wa mikopo.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mbinga, Paschal Zackaria Ndunguru, amehimiza wajasiriamali hao kutumia fursa ya tawi la NMB lililopo karibu ili kupata mikopo na kuendeleza biashara zao.
Amesisitiza kuwa kazi za mikono ni muhimu na ni chanzo kikubwa cha kipato, hivyo wajasiriamali wanapaswa kuwa waaminifu wanapochukua mikopo ili kujenga uaminifu kwa taasisi za kifedha.
Ndunguru pia amewapongeza akina mama wa kijiji cha Namswea kwa juhudi zao za kuuza zao la ndizi hadi mkoani Mtwara, jambo ambalo limeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.
Aidha, amebainisha kuwa biashara ya mahindi kutoka vijiji vya Kigonsera na Mkako inaweza kufanywa kwa ubunifu zaidi ili kuongeza thamani, ikiwemo kuuza mahindi ya kuchemshwa kwa kiwango bora zaidi.
Amesisitiza kuwa wajasiriamali wanapaswa kuungana na kushirikiana kwa karibu na viongozi wa serikali waliopo kwa ajili ya kuwasaidia.
Pia, amewataka kuepuka watu wanaoweza kuwavunja moyo na badala yake kuwa na mtazamo chanya kuhusu biashara zao.
Amewaonya dhidi ya kufungia vitambulisho hivyo ndani na badala yake wavitumie ipasavyo ili kufanikisha maendeleo yao.
Wakizungumza kwa niaba ya wajasiriamali wenzao, Anastazia Makubika na Joyce Hyera kutoka kijiji cha Kigonsera wametoa shukrani zao kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaunga mkono wajasiliamali wadogo.
Wameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo yao na kuleta maendeleo katika jamii zao.
Pia, wameeleza changamoto walizopitia hadi kufanikisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo, wakisisitiza kuwa watazitumia fursa walizopewa kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Bi Pendo Daniel akizungumza na wajasiriamali hao katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga
Social Plugin