Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUVUMA YAANDAA KUMBUKIZI YA MASHUJAA WA VITA VYA MAJIMAJI


Bango linaloonesha Makumbusho ya Vita ya Majimaji Songea
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Songea Mjini James Danny Mgego akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu kumbukizi ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji
Rose Kangu Kaimu Mfawidhi wa Makumbusho Mkoani Ruvuma akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ratiba za kumbukizi hizo za Mashujaa wa Vita ya Majimaji

Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 Blog Songea. 

Mkoa wa Ruvuma unajiandaa kwa kumbukizi maalum za Mashujaa wa Vita ya Majimaji, tukio muhimu la kihistoria linalolenga kuwaenzi wapigania uhuru waliopambana dhidi ya wakoloni wa Kijerumani mnamo mwaka 1906.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, James Danny Mgego, amesisitiza umuhimu wa kumbukizi hizi, akihimiza wakazi wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kuwaenzi mashujaa hao na kujua historia zao.

Rose Kangu, Kaimu Mfawidhi wa Makumbusho ya Majimaji, amewahimiza wananchi kuhudhuria kwa wingi maadhimisho haya ili kujifunza historia ya mashujaa wa Vita ya Majimaji na kuelewa mchango wao katika kupinga ukoloni.

Kulingana na ratiba ya maadhimisho hayo, kumbukizi zitaanza rasmi tarehe 23 mwezi huu, zikifuatwa na shughuli mbalimbali zinazolenga kudumisha utamaduni na historia ya mashujaa hao.

Tarehe 24, kutakuwa na mashindano ya ngoma za asili za utamaduni, ambapo vikundi mbalimbali vya sanaa vitashiriki kuonyesha tamaduni za wenyeji wa Ruvuma.

Tarehe 25, mdahalo mkubwa utafanyika Namtumbo, ukiwa na lengo la kujadili historia ya Vita ya Majimaji na umuhimu wake katika harakati za uhuru wa Tanganyika.

Tarehe 26, jamii ya Wangoni itakuwa na siku maalum ya kujifunza kuhusu tamaduni zao, ikiwa ni sehemu ya kurithisha mila na desturi kwa vizazi vya sasa.

Tarehe 27, itakuwa kilele cha kumbukizi, ambapo shughuli mbalimbali za heshima kwa mashujaa wa Vita ya Majimaji zitafanyika, ikiwa ni pamoja na kuelezea historia ya mashujaa hao waliopambana na hatimaye kunyongwa na wakoloni mwaka 1906.


Kumbukizi hizi ni tukio muhimu kwa wakazi wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla, likiwa na lengo la kutunza historia na kudumisha urithi wa mashujaa wa Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com