Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKAZI WA UKIMO MBINGA WAMEIPONGEZA SERIKALI KWA MRADI WA MAJI SAFI

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ukimo Kata ya Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma wakichota Maji baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)kufikisha maji ya bomba katika kijiji hicho

Na Regina Ndumbaro - Malunde 1 Blog,Mbinga 

Wakazi wa Kijiji cha Ukimo, Kata ya Mbangamao, Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwapatia mradi wa maji safi na salama ambao umemaliza adha ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofadhiliwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wananchi wamesema mradi huo utaboresha maisha yao kwa kiasi kikubwa, huku wakiahidi kuulinda ili uwanufaishe wao na vizazi vijavyo.

Regina Ndunguru, mkazi wa Kijiji cha Ukimo, amepongeza juhudi za RUWASA ngazi ya wilaya na mkoa kwa kutekeleza mradi huo ambao utamaliza changamoto ya kuchota maji kwenye vyanzo visivyo salama na umbali mrefu, hali iliyokuwa ikiwasababishia usumbufu mkubwa na kuhatarisha maisha yao kutokana na hatari kama vile kung’atwa na nyoka.

 Aliongeza kwakusema kuwa mradi huo utawapunguzia gharama ya maisha kwani awali walilazimika kununua ndoo moja ya maji ya lita 20 kwa Shilingi 1,000.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ukimo, Kanuni Mbunda, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za mradi huo, akisema upatikanaji wa maji shuleni utaondoa changamoto ya wanafunzi kuahirisha masomo ili kutafuta maji, na hivyo kuboresha mazingira ya kujifunza na usafi shuleni. 

"Maji haya yatatusaidia kuepuka magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhakikisha wanafunzi wanajisaidia na kunawa mikono kwa usahihi," amesema Mwalimu Mbunda.

Upendo Mbunda, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ukimo, amesema awali walikuwa wanachelewa kufika shuleni kwa sababu walilazimika kwenda mtoni kuchota maji kwa ajili ya shughuli za nyumbani kabla ya kuelekea shuleni, hali iliyochangia kushuka kwa ufaulu. 

Hata hivyo, ameeleza kuwa sasa wataweza kuwahi masomo na kutekeleza majukumu yao kwa wakati kutokana na upatikanaji wa maji karibu na makazi yao.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbinga, Mashaka Sinkala, amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi milioni 30 umetokana na fedha zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maji. 

Amefafanua kuwa mradi huo unatumia chanzo cha chemchem ya asili kilichoboreshwa na unahusisha ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji, vituo vya kuchota maji, na ulazaji wa mabomba kutoka chanzo hadi kwa wananchi. 

Sinkala amebainisha kuwa mradi huo utapunguza magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama na kuboresha huduma ya maji safi kwa wakazi wa Ukimo.

Wakazi wa Ukimo wameelezea matumaini yao kuwa mradi huo utaboresha hali ya maisha kijijini hapo, huku wakiahidi kushirikiana na Serikali kuulinda na kuutunza kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com