Na Regina Ndumbaro – Malunde 1 Blog, Songea
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeendelea na kampeni yake ya matumizi salama ya nishati ya umeme, likiwaangazia wananchi wa mitaa ya Chandarua na Mitendewawa katika kata ya Mshangano, Manispaa ya Songea Mjini, hatua ambayo imepokelewa kwa furaha na shukrani kubwa.
Diwani wa kata ya Mshangano, Samweli Mbano, ameishukuru TANESCO kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wa mitaa hiyo wanapata huduma ya umeme, huku akifafanua kuwa jumla ya transfoma mbili zimefungwa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Akizungumza kuhusu usalama na utunzaji wa miundombinu ya umeme, Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO mkoani Ruvuma, Allan Njiro, amekemea vikali vitendo vya wizi wa nyaya za umeme vinavyofanywa na baadhi ya watu, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweka hatarini maisha ya wananchi na kuvuruga huduma za umeme.
Njiro pia amewataka wazazi kuwa makini kwa kuhakikisha watoto hawachezi karibu na maeneo yenye transfoma za umeme ili kuepusha ajali, huku akisisitiza tahadhari wakati wa kukata miti iliyo karibu na nyaya za umeme, akibainisha kuwa usalama wa wananchi ni jambo la kipaumbele kwa TANESCO.
Aidha, Njiro amewaomba wananchi kushirikiana na TANESCO katika kulinda miundombinu ya umeme, huku akifafanua kuwa hakuna gharama za ziada zitakazotozwa zaidi ya zile rasmi zinazotolewa na shirika, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini na matapeli wanaoweza kujitokeza kudai fedha kinyume cha taratibu.
Afisa Msaidizi wa Habari na Mawasiliano wa TANESCO Ruvuma, Bi Emma Ulendo, ameeleza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme kwa wananchi ni shilingi 321,000 kwa kila kaya, ambapo kila mwananchi atapatiwa namba ya malipo (Control Number) kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuunganishiwa umeme majumbani mwao.
Wananchi wa mitaa hiyo wameeleza kufurahishwa na huduma ya umeme waliyoipokea, wakilishukuru shirika la TANESCO kwa kuzingatia mahitaji yao na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo yao.
Pamoja na shukrani zao, wananchi wameahidi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuunganishiwa umeme kwa kujaza fomu zinazotolewa na shirika hilo, wakibainisha kuwa hatua hiyo itaimarisha maisha yao na kutoa fursa zaidi za kufanya shughuli za kibiashara na maendeleo ya kiuchumi.
Huduma hii ya umeme si tu inaleta mwanga majumbani bali pia inatoa fursa mpya kwa wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kuimarisha uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla.
Social Plugin