
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkurumusi Casian Joseph Kayombo kata ya Mpitimbi akionyesha maeneo yasiyofikiwa na nguzo za umeme katika ziara hiyo ya utoaji elimu ya kufanya maombi ya kupata umeme



Wananchi waliojitokeza kupata elimu ya namna ya kufanya maombi ya kupata umeme Mkurumusi
Na Regina Ndumbaro, Mpitimbi-Songea
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya umeme.
Kampeni hii inalenga kuwafahamisha wananchi kuhusu utunzaji wa miundombinu ya umeme na utaratibu wa kufanya maombi ya kupata huduma hiyo muhimu.
Katika ziara iliyofanyika kijiji cha Mkurumusi, Kata ya Mpitimbi, wakazi wa eneo hilo walipewa elimu juu ya namna bora ya kutunza miundombinu ya umeme.
Aidha, walipewa maelekezo ya jinsi ya kuomba umeme kupitia njia za kidigitali kwa kutumia simu janja.
Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO mkoani Ruvuma, Allan Njiro, ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kulinda miundombinu ya umeme kwa kuepuka vitendo vya hujuma kama vile wizi wa mafuta ya transfoma na nyaya za umeme aina ya kopa.
Pia, amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwa waangalifu na kuhakikisha hawakati miti kiholela katika maeneo yaliyo na transfoma ili kuepusha uharibifu wa miundombinu.
Njiro ameeleza kuwa maombi ya umeme yanaweza kufanywa kupitia mitandao ya simu , kuhakikisha unakua na namba ya NIDA.
Kabla ya kuomba umeme, wananchi wanapaswa kuhakikisha nyumba zao zimefanyiwa wiring na kuna nguzo za umeme zinazofikika.
Kwa mujibu wa Njiro, gharama ya kupata umeme kwa wananchi wa vijijini ni shilingi 27,000 kwa njia moja, huku gharama ya njia tatu kwa matumizi ya viwanda ikiwa ni shilingi 139,000.
Amesisitiza kuwa TANESCO haitatoza gharama nyingine yoyote kwa huduma hiyo, ila mwananchi atapaswa kugharamia vifaa vya ndani kama soketi, balbu na mainswitch.
Kaimu Afisa Habari na Huduma kwa Wateja, Emma Ulendo, ameeleza kuwa umeme ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Pia amewataka wananchi kuhakikisha wanatekeleza hatua zote muhimu za kupata umeme, ikiwa ni pamoja na kufanya wiring kwenye nyumba zao.
Amesema kuwa kwa wakazi wa mijini, gharama ya kupata umeme ni shilingi 321,000 tofauti na vijijini ambako gharama ni shilingi 27,000.
Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kuuliza maswali walitaka kufahamu jinsi gani nguzo zilizo nje ya kilomita 30 zinaweza kufikishiwa huduma ya umeme.
Akijibu swali hilo, Emma Ulendo amesema kuwa serikali na TANESCO wanaendelea na mpango wa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mkurumusi, Casian Joseph Kayombo, kwa niaba ya Diwani wa Kata ya Mpitimbi, Mheshimiwa Issa Kindamba, amewasilisha ombi kwa TANESCO kuhakikisha wanawaharakishia huduma ya umeme wakazi wa eneo hilo.
Pia ametoa wito kwa wale ambao nguzo za umeme bado hazijawafikia, waangaliwe kwa upendeleo ili wapate huduma hiyo kwa haraka.
Aidha, Kayombo ameipongeza serikali ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya umeme.
Pia ametoa shukrani kwa Mbunge wa Songea Vijijini, Mheshimiwa Jenista Mhagama, ambaye pia ni Waziri wa Afya, kwa juhudi kubwa anazofanya katika kuwahudumia wananchi wake.
Kwa ujumla, wananchi wa Mpitimbi wamepokea kwa furaha taarifa za kuletwa kwa umeme katika maeneo yao, huku wakiahidi kushirikiana na TANESCO kulinda miundombinu na kutoa taarifa za wahalifu wanaojihusisha na uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Social Plugin