Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MRADI WA REA WA UJAZILIZI UMEME WAWAFIKIA WANANCHI WA NAMAKINGA NA DODOMA, RUVUMA

Afisa Habari na Uhusiano Tanesco Mkoani Ruvuma Allan Njiro akizungumza na Wananchi wa mtaa wa Namakinga na Dodoma Kata ya Maposeni Peramiho
Diwani wa kata ya Maposeni Bi Monica Tambara
Kaimu Afisa Habari na huduma kwa wateja Emma Ulendo akizungumza na wananchi wa kata ya Maposeni
Wananchi waliojitokeza kusikiliza maelekezo ya mradi jazilizi wa REA kata ya Maposeni mtaa wa Namakinga na Dodoma

Na Regina Ndumbaro - Ruvuma

Wananchi wa mitaa ya Namakinga na Dodoma, katika Kata ya Maposeni na Kata ya Peramiho, mkoani Ruvuma, wamepokea kwa shukrani mradi wa ujazilizi wa umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Wakazi wa maeneo hayo wameeleza furaha yao kwa Serikali, wakitambua mchango mkubwa wa mradi huu katika kuboresha maisha yao.


Afisa Habari na Uhusiano wa TANESCO mkoani Ruvuma, Allan Njiro, amewatembelea wananchi wa mitaa hiyo na kuwapa elimu muhimu kuhusu taratibu za kupata huduma ya umeme.


Amesema mradi huu ni wa gharama nafuu, ambapo wananchi wanaounganishiwa umeme kwa matumizi ya nyumbani wanapaswa kulipa shilingi 27,000, huku wale wanaohitaji kwa matumizi ya viwanda wakitakiwa kulipa shilingi 139,000.


Aidha, Njiro amefafanua kuwa wananchi wanaotaka kuunganishiwa umeme wanapaswa kufanya maombi kwa njia ya simu, kuwa na kitambulisho cha NIDA, kuhakikisha kuwa wiring ya nyumba zimekaguliwa na mkandarasi , na kuhakiki uwepo wa nguzo za umeme .

Pia, ameeleza kuwa gharama za vifaa vya ndani kama soketi, balbu, mainswitch na vifaa vingine ni jukumu la mwananchi mwenyewe, huku akisisitiza kuwa ada ya kuunganishiwa umeme inabaki kuwa bure.


Katika juhudi za kuhakikisha miundombinu ya umeme inalindwa, Njiro amewataka wananchi kushirikiana katika kulinda transfoma, waya za umeme, na vifaa vingine vya umeme.


Amesisitiza kuwa yeyote anayehisi kuna mtu anayehusika na wizi au uharibifu wa vifaa hivyo asisite kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kuhakikisha huduma hiyo inaendelea kutolewa bila changamoto.


Kwa upande wake, Kaimu Afisa Habari wa Huduma kwa Wateja, Emma Ulendo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hii ya ujazilishi wa umeme kwa manufaa ya jamii.


Amesema kuwa ni muhimu kwa wakazi kuhakikisha wanafanya wiring ya nyumba zao kwa gharama elekezi ya mkandarasi na pia gharama za kulipia umeme huo kwa wananchi wa Songea Vijijini ni shilingi 27,000 ambapo kwa wale wanaoishi mjini gharama yake inabaki ile ile ya shilingi 321,000 kuwezesha uunganishwaji wa umeme kwa haraka na kwa usalama.


Diwani wa Kata ya Maposeni, Monica Tambara, ameipongeza TANESCO mkoani Ruvuma kwa kuwapatia elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa miundombinu ya umeme.


Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu.


Tambara pia amempongeza Waziri wa Afya na Mbunge wa Songea Vijijini, Mhe. Jenista Mhagama, kwa juhudi zake katika kuhakikisha maendeleo ya wananchi wa Songea yanaimarika.


Ameiomba Serikali kuhakikisha kuwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na mradi huu wa ujazilishi wa umeme yanapatiwa huduma hiyo haraka iwezekanavyo.


Mradi huu wa REA unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wakazi wa Namakinga na Dodoma, huku ukiwa chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara, elimu na afya.


Serikali inaendelea kusisitiza ushirikiano wa wananchi katika kuutunza mradi huu, ili kuhakikisha unawanufaisha kwa muda mrefu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com