Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI YA NYASA KUKUSANYA SH. BILIONI 29.9 KWA AJILI YA MAENDELEO

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Mkoani Ruvuma Khalid Khalifa akizungumza na Watumishi na Madiwani kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri .
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri pichani hayupo katika mpango wa rasimu ya Bajeti ya 2025/26
Mwenyekiti Wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Stewart Nombo akifungua kikao kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri na kulia kwake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Khalid Khalifa
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la kupitisha rasimu ya Mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2025/26.

Na Regina Ndumbaro-Mbambabay, Nyasa.

 Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, imepanga kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 29.9 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni 17.144 zitatumika kwa ajili ya mishahara, Shilingi bilioni 4.4 kwa matumizi mengineyo, na Shilingi bilioni 8.319 kwa miradi ya maendeleo, ambapo Shilingi bilioni 4.020 ni fedha za ndani.

Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri hiyo, Christopher Ngonyani, ameeleza hayo wakati akiwasilisha mpango wa bajeti kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri mjini Mbambabay. 

Amesema kuwa bajeti hiyo imelenga kuboresha sekta mbalimbali muhimu kwa maendeleo ya wananchi.

Kwa mujibu wa Ngonyani, fedha za maendeleo za nje zinatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 4, huku mapato ya ndani ya Halmashauri yakikadiriwa kufikia Shilingi bilioni 2.9. Kati ya mapato ya ndani, Shilingi bilioni 1.7 ni mapato halisi, Shilingi milioni 1.056 ni mapato linda, na Shilingi milioni 341.366 ni fedha za miradi ya maendeleo.

Bajeti hiyo imeweka vipaumbele katika kuboresha miundombinu ya elimu na afya, pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama kahawa, ufuta, na kokoa. Ili kufanikisha mkakati huo, Halmashauri imetenga Shilingi milioni 60 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu za mazao hayo, ambazo zitagawiwa bure kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na mapato ya Halmashauri kupitia ushuru wa mazao.

Katika sekta ya utawala, Halmashauri imetenga Shilingi milioni 60 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi za serikali za vijiji na kata. 

Lengo ni kuimarisha utawala bora na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watendaji wa serikali, ili wananchi wapate huduma bora kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, amewataka madiwani, watendaji wa kata, na watumishi wa Halmashauri kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuvisimamia kwa ufanisi. 

Amesisitiza kuwa makadirio ya Shilingi bilioni 2.9 yanahitaji juhudi za pamoja ili kufikiwa na kwamba kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Magiri amesisitiza kuwa fedha hizo zitasaidia kuongeza uwezo wa Halmashauri kujitegemea na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yote ya Wilaya ya Nyasa.

 Amewataka madiwani kushirikiana kwa karibu na wananchi ili kufanikisha mipango iliyopangwa kwa mwaka wa fedha ujao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyasa, Stewart Nombo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuipatia Wilaya hiyo fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

 Amesema kuwa fedha hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Nyasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com