Na WAF - KAHAMA
Msajili wa Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi amevitaka vituo viwili vya utoaji huduma ya macho vilivyoko Manispaa ya Kahama Shinyanga kuwaondoa mara moja vishoka wawili wa taaluma ya Optometria waliokuwa wakifanya kazi katika vituo hivyo.
Vishoka hao wamebainika kufanya kosa la kufanya kazi kinyume cha sheria ya Baraza hilo namba 23 ya mwaka 2007 hivyo kuwataka kutojihusisha na kazi ya kutengeneza miwani. Vishoka hao wanatoka vituo vya CVT na Sight Plus Optometry vyote vya Manispaa ya Kahama.
Bw. Millanzi amechukua hatua ya kuwa ondoa Said Msabaha wa CVT Specialized Clinic pamoja naye Idd Jummanne wa Sight Plus Optometric Clinic tarehe 25, Februari 2025 wakati wa zoezi la Usimamizi Shirikishi linalofanyika katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
"Sheria ya Baraza inataka kila anayetekeleza shughuli za Optometria kwanza awe ni mtaalam lakini pili awe na Leseni hai inayotambuliwa na Baraza" ,amesema Millanzi.
Aidha vishoka hao walikiri kupata ujuzi huo kutoka kwa baadhi ya wataalam wa optometria katika vituo tofauti vya kutolea huduma za optometria mkoani Mwanza na Dar-es-salaam.
Kufuatia maelezo yao hayo kwa nyakati tofauti Bw. Millanzi aliwataka vishoka hao kuacha mara moja kuvunja Sheria ya Optometria Sura ya 23 kwa kuachana mara moja walichokuwa wanakifanya, kwani kuendelea kufanya hivyo ni kwenda kinyume hali inayohatarisha afya ya macho ya wananchi.
Pamoja na maagizo hayo Bw. Millanzi ametoa wito kwa wataalam wa optometria nchini kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Optometria Sura ya 23, ikiwemo kutokutoa maarifa ya optometria kwa watu wasiotajwa katika Sheria hiyo kama kifungu cha 37 cha Sheria ya Optometria kinavyokataza.
"Vituo vya kutolea huduma vitakavyobainika kuajiri wafanyakazi wasiosajiliwa vitachukuliwa hatua kali za kisheria pamoja na kufungiwa kutoa huduma na faini mbalimbali" amefafanua Bw. Millanzi.
Wamiliki wa vituo hivyo walivyotakiwa kueleza vigezo gani vilitumika kuwapa ajira ya kitaalamu vishoka hao walikosa maelezo ya kutosha, huku wakisema wao walizingatia uzoefu wao pasipo kuwasilisha vyeti vya kitaaluma.
Hata hivyo ilimlazimu Msajili wa Baraza kuwaamuru wamiliki wa vituo hivyo kuchukua hatua stahiki ikiwepo ya kutafuta wataalam wenye taaluma ya Optometria waliosajiliwa na Baraza ili shughuli zao za kutoa huduma kwa jamii ziweze kuendelea ikiwepo utengenezaji wa miwani.
Social Plugin