Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA IMEJIPANGA MAANDALIZI CHAN NA AFCON - MAJALIWA




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga vyema kukamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo miundombinu kwa ajili ya Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Africa CHAN na AFCON.

"Tanzania imejipanga vizuri, kuhakikisha kuwa michuano hii inafanyika hapa Nchini, Serikali inawajibika kuhakikisha inaandaa viwanja na miundombinu mingine."

Ameyasema hayo leo (Jumamosi Februari Mosi, 2025) aliposhiriki katika Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.

Amesema kuwa tayari ukaguzi wa baadhi ya viwanja umefanyika na vimeonekana kukidhi vigezo “Viwanja vilivyokaguliwa vipo Tanzania bara na Visiwani, na kazi bado inaendelea, lengo ni kuhakikisha michuano hii inafanyika kwa ufanisi”

Amesema ni vyema sasa Watanzania wakajipanga kutumia fursa zitakazo jitokeza kutokana na kuwepo kwa michuano hiyo hapa Nchini. "Hii ni fursa kwetu Watanzania, lazima tujipange kutumia fursa za kiuchumi zitakazojitokeza, ili tuweze kunufaika".

Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu amempongeza Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson kwa kuandaa Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza ambalo limewakutanisha wabunge na wanamichezo mbalimbali wa Mkoani Dodoma.

"Tamasha hili limekuwa na mafanikio makubwa, limetupa nafasi wabunge kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali pamoja na kuimarisha afya zetu."

Amesema ni vyema Watanzania wakaendelea na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bunge bonanza Festo Sanga amesema bonanza hilo ni sehemu ya mafaniko katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

"Tumeona ubora wa bonanza hili na tunawashukuru sana Azania Bank
kwa mchango wake hadi kufanikisha kila kitu, hatutaishia hapa tutafanya bunge marathon tena kuchangia ujenzi wa shule ya wavulana, " amesema


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com