Na Regina Ndumbaro – Ruvuma
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Songea Mhifadhi Issa Mlela, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda na kuhifadhi misitu ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mlela amesisitiza kuwa misitu ni rasilimali muhimu kwa maisha ya binadamu, uchumi, na ekolojia kwa ujumla.
Amebainisha kuwa uharibifu wa misitu unachangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi na ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula.
Kwa mujibu wa meneja huyo, TFS imeweka mikakati madhubuti ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa misitu kwa kutumia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara, na kushirikiana na viongozi wa kijamii.
"Tunataka kila mwananchi aelewe thamani ya misitu na athari za uharibifu wake, ndiyo maana tumejikita katika kutoa elimu ili kuongeza uelewa kwa jamii," amesema.
Katika kuhakikisha misitu inalindwa ipasavyo, Mhifadhi Mlela amesema kuwa TFS imeimarisha doria za mara kwa mara ili kudhibiti ukataji miti holela,uchomaji wa moto wa misitu, na uingizaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Aidha, ameeleza kuwa usimamizi endelevu wa misitu unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wadau wa mazingira, na jamii kwa ujumla.
Akizungumzia faida za misitu, Mlela ameeleza kuwa misitu inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhifadhi vyanzo vya maji, kupunguza joto, na kusaidia katika uzalishaji wa hewa safi.
"Misitu siyo tu kwamba inatupatia hewa safi, bali pia ni chanzo cha mbao, matunda, dawa za asili, na hifadhi ya viumbe hai. Hivyo, ni lazima tuilinde kwa gharama yoyote," amesema.
Katika juhudi za kuhifadhi misitu, TFS imekuwa ikiendesha kampeni za upandaji miti kila mwaka ili kurejesha uoto wa asili na kuimarisha mifumo ya ekolojia.
Mlela amesema kuwa mwaka huu, kampeni hiyo imefanikiwa kupanda miti million moja na laki tano katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma, hususan katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Manispaa ya Songea, huku wananchi wakihamasishwa kushiriki kikamilifu.
Aina za miti iliyopandwa katika kampeni hiyo ni pamoja na miti ya mbao na miti ya kivuli na matunda.
"Tunapanda miti kulingana na mazingira na mahitaji ya jamii husika ili kuhakikisha miti hiyo inakua kwa ufanisi na kuleta manufaa kwa wananchi",amesema.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na TFS katika kulinda misitu kwa kuepuka ukataji miti hovyo, uchomaji moto wa misitu, na uharibifu wa vyanzo vya maji.
"Utunzaji wa misitu ni jukumu la kila mmoja wetu. Tukishirikiana, tutaweza kuhakikisha rasilimali hii inabaki salama kwa sasa na kwa vizazi vijavyo,"ameongeza
Social Plugin