Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SGR KUUNGANISHA TANZANIA NA BURUNDI


Na Mwandishi Wetu,  DAR ES SALAAM.

SHIRIKA la Reli la Tanzania - TRC chini ya Wizara ya Uchukuzi limesaini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha 7 na 8 kutoka Uvinza nchini Tanzania hadi Musongati nchini Burundi chenye urefu wa kilomita 282 ambapo kilo MITA 240 ni za njia kuu na kilomita 42 ni za njia za kupishania.

Mkataba huo umesainiwa januari 29, 2025 katika stesheni ya SGR John Pombe Magufuli, jijini Dar es Salaam, baina ya Serikali ya Tanzania kupitia TRC, Serikali ya Burundi kupitia Wizara ya Miundombinu na muungano wa kampuni za CREGC (China Railway Engineering Group Co. LTD) na CREDC (China Railway Engineering Design and Consulting Group Co. LTD) za nchini China.

 Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kupitia utiaji saini wa mkataba huu, anawapongeza marais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Burundi kwa kuweka historia ya utekelezaji wa vitendo wa Ajenda ya Umoja wa Afrika 2026 ya kuunganisha nchi za Afrika kwa reli ya kisasa.

Amesema mkataba huo utagharimu kiasi cha Dola za marekani bilioni 2.154 na muda wa utekelezaji wake ni miezi 72 ikijumuisha na muda wa matazamio wa miezi 12.

Amebainisha kuwa mradi  utajenga daraja  linalounganisha Tanzania na Burundi lililosanifiwa kubeba reli na Barabara lenye urefu wa kilomita moja na stesheni zipatazo saba na kituo cha mizigo kimoja katika eneo la Musongati na usanifu wa ujenzi huu tumezingatia viwango vinavyotumika katika ujenzi wa vipande vingine vinavyojengwa nchini Tanzania. 

"Mradi huu unavipande viwili ambapo kipande cha kwanza ni Uvinza - Malagarasi chenye urefu wa kilomita 180 na kipande cha pili ni kutoka Malagarasi hadi Musongati chenye urefu wa kilomita 102 kwa garama ya Trilioni 5.6 za kitanzania. 

Pia, Prof. Mbarawa ameongeza kuwa ujenzi wa reli ya kimkakati umekua ukitoa fursa za ajira kwa Watanzania pamoja na zabuni mbalimbali katika ujenzi wa SGR unaoendelea nchini kwani zaidi ya wafanyakazi elfu thelathini wamepata ajira.

"Lakini  pia umewezesha kuingiza kipato cha zaidi ya bilioni mia tatu hamsini za Kitanzania na kutoa kandarasi ndogo za Watanzania zenye thamani ya shilingi za kitanzania takribani trilioni 3.7.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema utiaji saini wa mkataba huu wa ujenzi wa kipande cha saba na nane ni muendelezo wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa awamu ya pili baada ya kusainiwa kwa kipande cha sita akutoka Tabora - Kigoma mwezi Disemba 2022 na hivyo kufanya kuwa na utekelezaji wa vipande vitatu kati ya vipande vinne vya ujenzi wa reli ya awamu ya pili. 

Aidha, Ndugu Kadogosa ameongeza kuwa TRC inatelekeza kauli ya Mheshimiwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuiunganisha Tanzania, Burundi na DRC, TRC inaendelea na utekelezaji wa kipande cha Tabora hadi Kigoma.

"Na hivi sasa umefikia asilimia 7.12 na hii inafanya utekelezaji wa mradi huu kufanyika kwa vipande vyote kuanzia Dar es salaam hadi Kigoma na kuwezesha kipande cha Uvinza - Musongati,

"Kwa sasa DRC na Burundi wanaendelea na upembuzi yakinifu kwaajili ya ujenzi wa reli kati ya Musongati na Kindu (DRC)", amesema Kadogosa.

Mwakilishi kutoka kampuni CREGC na CREDC ameushukuru Serikali ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa kampuni hizi kwenye ujenzi wa reli ya SGR kipande cha Uvinza hadi Musongati itakayoleta tija na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii baina ya Tanzania na Burundi.

"Kwa miaka 50 iliyopita kampuni hizi zimejenga kilomita 1560 za reli ya TAZARA kwa ufanisi mkubwa, zimejenga madaraja makubwa Afrika na hii imefanya Afrika kuwa rafiki mkubwa wa nchi ya China miongoni mwao ikiwa Tanzania" ameongeza Mwakilishi wa CREGC   & CREDC.

Mnamo tarehe 28 Januari 2022, Tanzania na Burundi zilisaini makubaliano ya ushirikiano wa ujenzi wa reli  kati ya Uvinza nchini Tanzania na Musongati ya nchini Burundi na TRC ilipewa jukumu la kufanya ununuzi wa mkandarasi na kusimamia ujenzi wa mradi husika kwa niaba ya nchi zote mbili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com