Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA YATAKA WATU WENYE ULEMAVU KUWASILISHA MALALAMIKO


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imewataka watu wenye ulemavu kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika Ofisi za Tume ili kupatiwa ufumbuzi.


Wito huo umetolewa na Afisa Uchunguzi Mkuu Bi. Eugenia Lohay alipokuwa akitoa elimu ya haki za binadamu kwa watu wenye ulemavu katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma  leo tarehe 27 Januari 2025.

Bi. Lohay amesema kuwa watu wenye Ulemavu hawapaswi kutengwa wala kunyanyaswa kwa kuwa wanahaki sawa na binadamu wengine hivyo kwa Chochote wanachopitia ambacho ni ukiukwaji wa haki za binadamu wanapaswa kutoa taarifa katika Mamlaka husika na kupatiwa msaada wa kisheria.

" Tunapokea malalamiko ya kila mtu, yanayohusiana na uvunjifu wa haki za binadamu, haijalishi umefanyiwa na nani na katika mazingira gani hivyo ni jukumu letu kwa pamoja kupinga unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya watu wenye ulemavu" Amesema Bi. Lohay.


Pia, Bi. Lohay ameeleza njia ambazo Tume hutumia kupokea malalamiko ikiwa ni pamoja na kuandika barua,  kufika ofisini, kupitia tovuti ya Tume na simu ya kiganjani.

Kwa niaba ya Watu wenye ulemavu Bw. Hussein Ramadhani Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye  Ulemavu ameishukuru Tume kwa kuwapiatia elimu hiyo na kuwa msaada mkubwa kwani kumekuwa na watu wengi wanaofika katika Ofisi za Tume na kuhudumiwa vizuri kwani malalamiko hayarudi tena kwenye Shirikisho.

Naye Katibu wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Dodoma Bi. Bhoke Ramadhani amesema kutokana na elimu hiyo  anakwenda kufanya jitihada katika kuwasaidia watu wengine kufika katika ofisi za Tume ya Haki za Binadamu.

 Aidha, Bi. Bhoke ametoa wito kwa Tume kuona namna ya  kusaidia  watu wenye ulemavu wa kusikia kuweza kupata haki zao kwa urahisi katika ofisi za umma kwa kuweka wakalimani.

Maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square  yamelenga kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi na kutoa elimu juu ya haki mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com