UJENZI WA KITUO CHA KUSHINDILIA NA KUJAZA GESI ASILIA KWENYE MAGARI WAFIKIA ASILIMIA 33.5


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

UJENZI wa Kituo cha Kushindilia na Kujaza gesi asilia (CNG) kwenye magari uliopo Ubungo Jijini Dar es Salaam unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, na hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 33.5.

Katika ujenzi huo, uundaji wa mitambo itakayokuja kusimikwa unaendelea kufanyika nchini China na tayari umefikia asilimia 76.

Akizungumza leo Agosti 21, 2024 Jijini Dar es Salaam, wakati akiongoza Bodi ya Wakurugenzi pamoja na menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mwenyekiti wa Bodi hiyo Balozi Ombeni Sefue amesema kituo hicho kitakuwa na pampu za kujaza gesi (gas dispensers) nne, na kila pampu itakuwa na nozeli mbili. 

"Hivyo kutakuwa na nozeli nane zenye uwezo wa kujaza CNG kwenye gari nane kwa mara moja. Vilevile, kituo kitakuwa na pampu maalum (loading gantry) tatu za kujaza gesi kwenye magari maalumu ya kubebea gesi asilia (CNG tube trailers) tayari kwa kusafirishwa". Amesema 

Amesema kituo hicho ni kituo mama cha kujaza na kusambaza gesi katika mikoa mbalimbali kwa kuanza na mikoa ya Dodoma na Morogoro pia kusambaza gesi katika vituo vingine vidogo vitakavyojengwa katika maeneo ya  Muhimbili na Kibaha mkoani Pwani. 

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuweka mifumo ya gesi asilia kwenye magari yao ama kununua magari yaliyoundwa tayari kutumia gesi asilia kwa kuwa mwarobaini wa kero ya upatikanaji wa vituo vya kujaza gesi asilia umepatikana.

Vilevile ametoa rai kwa wamiliki wa viwanda vilivyoko Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam kuchangamkia fursa hiyo ya CNG kwa matumizi mbalimbali, kama vile uzalishaji wa umeme na
kuendeshea mitambo kwani gesi itakuwa ikipatikana kwa hakika na urahisi zaidi kuliko
ilivyokuwa kabla.

"Miundombinu hii tunayoiweka, na hamasa hizi tunazozitoa kwa wananchi, hatima yake itakuwa
ongezeko kubwa la mahitaji ya gesi asilia. Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa TPDC imejipanga kuhakikisha kuwa tunaongeza kiasi cha gesi asilia kilichopo ili kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo, si kwa Tanzania tu bali kwa nchi za jirani vilevile". Amesema 

Kwa upande wake Meneja Msimamizi wa mradi wa Kituo hicho, Mhandisi Aristides Katto amesema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza gesi kwenye magari takribani 1,000 kwa siku na kwamba mradi huo utagharimu shilingi Bilioni 14.55 hadi kukamilika kwake.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza  changamoto iliyopo sasa ya upatikanaji wa nishati hiyo ambayo ina watumiaji wengi katika kuendeshea magari pamoja na viwanda na shughuli za majumbani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post