TANZANIA YASISITIZA KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA JAPAN ILI KUCHOCHEA MAENDELEO YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI


Tanzania imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na Japan pamoja na wadau wengine ili kuchangia maendeleo na hatimaye kuendelea kuimarika zaidi Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Msisitizo huo umetolewa na Mhe. Stephen L. Byabato (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa mazungumzo na Mhe. Yusushi Misawa, Balozi wa Japan nchini Tanzania.

Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali kuhusu maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Serikali ya Japan imekuwa mdau muhimu kuchangia maendeleo hayo. Japan imeshirikiana na Serikali ya Tanzania katika kujenga miradi ya Barabara, Maji, Vituo vya Huduma ya Pamoja Mipakani ( One Stop Border Post -OSBP), Mafunzo ya kuendeleza biashara kwa maafisa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya na ujenzi wa miundo mbinu ya Umeme. 

Akizungumza kwenye mazungumzo hayo, Mhe. Byabato ameishukuru serikali ya Japani kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla. Kadhalika, Mhe. Byabato ametoa wito kwa Japan kuona namna ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Upanuzi wa Barabara ya Kibaha-Chalinze-Morogoro kuwa njia sita ili kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuweza kuhudumia vyema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Burundi, DR Congo, Rwanda na Uganda ambayo ni tegemeo kwa nchi hizo.

Vilevile ameiomba Japan kuchangia ujenzi wa Mradi wa kusafisha umeme kutoka Zambia, Tunduma kwenda hadi Kenya;  ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, Wete, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam;  na ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili, Kyaka-Mtukula na miradi mingine ya Jumuiya ili kuiwezesha kuleta maendeleo yaliyokusudia ikiwemo kurahisisha ufanyikaji wa biashara,  uwekezaji, utalii na kuungana kama lilivyolengo mama la Jumuiya na Afrika kwa ujumla. 

 Kwa upande wake, Balozi wa Japan amepongeza juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha nchi za Afika zinaungana. Ameaidi kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania pamoja na nchi nyingine kwa maslahi mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia viongozi  hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Japan ambapo wamekubaliana kuendelea kushirikiana kwa ukaribu zaidi kwa maslahi ya pande zote mbili. Mhe. Byabato ameiomba Japan kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kukamilisha ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa hususani kipande cha Isaka-Mwanza, Isaka-Keza/Gitega na Isaka-Kigali ambayo itawezesha kuendelea kuimarika zaidi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mhe. Byabato amemuomba Balozi wa Japan akipata muda atembelee Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Arusha, Pia ushirikiano wa Tanzania na Japan ulianza tangu mwaka 1961.
   

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post