MFUMO WA PAMOJA WA UKUSANYAJI TOZO KUANZISHWA ILI KURAHISISHA UFANYAJI BIASHARA


Waziri wa Viwanda na Biashara,Mhe Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa mfumo mmoja wa ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara nchini ili kuondoa kero ya taasisi mbalimbali za Serikali kukusanya kodi.

Alitoa kauli hiyo Mei 10, 2024 jijini Mbeya wakati wa Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta umma na Sekta binafsi uliokuwa na lengo la kujadiliana namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara katika Mkoa huo.

Aidha. Dkt. Kijaji alisema kero hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali kuwa ilikuwa ikichangia kuua biashara na kufukuza wajasiriamali.

“Kilio hiki tumeshakisikia na kama Serikali tunaendelea na majadiliano ya kuanzisha mfumo mmoja wa kukusanya mapato, yatakusanywa kwenye kapu moja kisha kila taasisi itapata mgawo wake na hivyo kupunguza usumbufu,” alisema Dkt. Kijaji.

Aidha alisema Serikali za Tanzania na Marekani zimeanzisha chemba moja ya wafanyabiashara nchini marekani kwa lengo la kurahisisha ushirikiano wa biashara na kupunguza mlolongo wa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Vilevile aliwataka watanzania kuwa waaminifu kwenye biashara ili kuepuka kuharibu masoko ya kimataifa akidai kuwa fursa hiyo ya soko la marekani ni muhimu kulindwa pamoja na masoko mengine ya kimataifa.

Alisema wizara inaendelea na mazungumzo na Shirika la Ndege la Uturuki kwa ajili ya kuanza usafirishaji wa maparachichi yanayozalishwa nchini kwenda uturuki ambako kuna soko kubwa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah alisema Wizara hiyo imekuwa ikishirikiana na vyombo mbalimbali kufanya oparesheni za kukamata bidhaa bandia zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani na afya za wananchi.

Alisema hivi karibuni walifanya ukaguzi kwenye mikoa mbalimbali nchini na kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wakiuza simu feki na hivyo wakachukua hatua za kisheria ikiwemo kutaifisha bidhaa hizo na kuwasweka ndani wahusika.

Aliagiza taasisi zinazohusika na usimamizi wa ubora wa bidhaa nchini kuendelea kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka ili kukuza viwanda vya ndani na kulinda usalama wa wananchi.

“Hatuwezi kuacha watu wanaingiza bidhaa feki nchini, bidhaa hizo ni hatari kwa Uchumi wetu na kwa maisha ya wananchi, kwahiyo niwahakikishie kwamba tutaendelea kuchukua hatua maana usalama wa watanzania upo mikononi mwetu,” alisema Abdallah.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Chemba ya wafanyabiashara, viwanda na kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mbeya, Erick Sichinga alisema utitiri wa kodi umekuwa ukisababisha kutoelewana kati ya wafanyabiashara na taasisi za serikali.

Alisema baadhi ya taasisi zinazokusanya kodi na tozo zimekuwa zikifanya kazi bila kuwashirikisha watu wa sekta binafsi ili na wao watoe maoni yao hali ambayo inaendelea kusababisha migogoro.

Alisema moja kati ya taasisi ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA) ambazo zimekuwa zikiwatoza tozo kubwa.

Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Victoria Michael alisema baadhi ya Halmashauri na mikoa nchini imekuwa ikianzisha tozo mbalimbali ambazo zinakinzana na Mpango wa Kuboresha Mazingira ya biashara (MKUMBI).

Alisema lengo la mpango huo ni kutatua kero za kibiashara zinazowakumba wafanyabiashara lakini zinapoanzishwa tuzo mpya kwenye halmashauri ni uzalishaji wa matatizo mapya kinyume na lengo.

Victoria ambaye ni mchambuzi wa sera alisema sekta binafsi kwa sasa inachangia asilimia 50 na sekta ya umma inachangia asilimia 50 kwenye majadiliano ya kuboroesha mazingira ya biashara.

Ofisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Songwe, Elijah Simbeye alishauri serikali kutatua kero za kodi ikiwemo kuondoa utitiri wa kodi kwa kuziweka kwenye kapu moja ili kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post