CCM MORO YAITAKA CHADEMA KUACHA UPOTOSHAJI KWA WANANCHI

 

Na Christina Cosmas, Morogoro

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Morogoro kimeutaka uongozi wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kuacha tabia ya upotoshaji kwa wananchi ikiwemo mchakato wa ukusanyaji maoni ya katiba mpya wa Tume ya Jaji Warioba kwa kuingiza misimamo isiyothabiti ya uwepo wa Serikali ya Tanganyika jambo ambalo si kweli.


Katibu wa Siasa, Uenezi na mafunzo CCM mkoani hapa Zangina Shanang Zangina alisema hayo jana wakati akiongea na vyombo vya habari kwenye ofisi za CCM mkoa wa Morogoro ambapo alisema kauli za upotoshaji zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu wakati wa mkutano baada ya maandamano mwishoni mwa mwezi Aprili hazivumiliki kuzinyamazia.


Alisema watanzania wanapaswa kutambua kuwa mpango wa Serikali ya Tanganyika uliibuka kwenye katiba ya Tume ya Jaji Warioba kwa kuwa UKAWA waliubaka mchakato wa tume hiyo na kuiaminisha kuwa ilikuwa inakusanya maoni ya wananchi lakini kiuhalisia CHADEMA ilipita kila mkoa kupandikiza watu ili waingize misimamo yao.


Hivyo aliwataka CHADEMA kuacha kulazimisha kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika itakayoongeza mzigo wa kodi kwa watanzania sababu Serikali mbili zinatosha ambapo alisema kama wanataka Serikali tatu waanze na kubadilisha kwenye salamu yao kwa kuonesha vidole vitatu badala ya viwili na sio kuwarubuni wananchi.


Zangina alisema agenda ya uwepo wa Serikali ya tatu ya Tanganyika kuwa ni TAMISEMI sio hoja ya msingi sababu haipo na TAMISEMI ni Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa ambayo ipo ndani ya Serikali Tanzania.


Aliitaka CHADEMA kutolazimisha agendaya serikali tatu ionekane ni hitajio la wananchi wakati ni mpango wa CHADEMA wa kuongeza utitiri wa Madaraka na kutaka kujiimarisha kisisasa na kisha kuuvunja muungano wa kuwa wamejaa roho ya ubaguzi kwa Zanzibar.


Hivyo aliishauri CHADEMA kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza vyema dhana ya maridhiano na vyama vya upinzani na kuacha kushutumu sababu maandamano na mikutano wanayofanya ni sehemu ya utekelezaji wa maridhiano yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post