ZINAHITAJIKA JUHUDI NA NGUVU YA PAMOJA KUSHUGHULIKIA CHANGAMOTO YA UHAMIAJI HARAMU - CHIEF CHARUMBIRA

Mhe. Chifu Fortune Charumbira


Na Moshi Ndugulile

Rais wa Bunge la Afrika Chief Fortune Charumbira amesema Bunge hilo lina wajibu mkubwa wa kukuza na kuimarisha misingi ya haki za binaadamu, demokrasia na utawala bora , uwazi pamoja na uwajibikaji katika Nchi wanachama barani Afrika,hasa katika hatua za kushughulikia uhamiaji.

Ameyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Uhamiaji wa Euro-Afrika Mjini Benghazi Nchini Libya ambapo ametaka kuweka umadhubuti kuhakikisha kunakuwa na uhamiaji wenye manufaa kwa pande zote kupitia sera na mipango baina ya maeneo husika.

Chief Charumbira ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine Mkutano huo umelenga kujadili na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto ya uhamiaji kuvuka na kuingia Italia na Malta kupitia Libya, ili kuondokana na athari za uhamiaji haramu,hivyo kukuza zaidi Amani,usalama, utulivu, ushirikiano na maendeleo barani Afrika.

Ameeleza zaidi kuwa hatua hiyo imelenga kukabiliana uhamiaji haramu ambao umekuwa ukisababisha athari kwa raia ambao wanafanya biashara halali.

“Kwa kuzingatia ukweli kwamba, hivi karibuni, Libya ilikuwa sehemu kuu ya kuondoka wahamiaji kuelekea bara la Ulaya,na kwamba tangu wakati huo Tunisia imeipiku Libya kwa zaidi ya asilimia 62% ya watu zaidi ya 150 000 waliovuka Katika eneo la Mediterranean kwa kutumia usafiri wa boti mwaka 2023”.

“Njia ya kati ya Mediterania (njia ya kutoka Algeria, misri, Libya na Tunisia hadi Italia na malta) imerekodi angalau vifo 3 na kupotea kwa watu 129 mnamo mwaka 2023,” ameeleza Chief Charumbira.

Ametaka kukomeswa kwa matumizi ya silaha na badala yake kuimarisha ushirikiano ,umoja na mshikamano wa kidiplomasia baina ya Ulaya na Afrika kwa mstakabali mwema wa Amani na usalama.

Ametaka kuwepo ushirikiano zaidi baina ya bara la Afrika na Ulaya katika hatua zote za kukabiliana na suala hilo,huku akiutaja umaskini kama chanzo cha uhamiaji haramu ambapo ameomba juhudi zaidi zitakazowezesha kuondoa hali hiyo.

Kongamano hilo limeanza Mei 25,2024 na litahitimishwa Mei 27,2024 kufikiwa kwa maazimio kuhusu uhamiaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post