WAKULIMA 640 WA MPUNGA WASISITIZWA KUACHA KILIMO CHA KIZAMANI Na Christina Haule, Morogoro

WAKULIMA 640 wa mpunga Wilayani Kilombero mkoani Morogoro wamesisitizwa kuachana na kilimo cha kizamani bali watumie pembejeo na zana za kilimo za kisasa ili kupata manufaa ya kilimo na kuleta tija kwao na Taifa kwa ujumla.

Meneja masoko wa kampuni inayojihusisha na uuzwaji wa bidhaa za kilimo (HUGHES Agricultural Ltd) Bonifasi Mollel alisema hayo jana wakati akitoa mada ya umuhimu wa pembejeo bora za kilimo kwa wakulima wa mpunga kwenye mafunzo ya kilimo bora yaliyoandaliwa na Serikali, kampuni ya pembejeo ya HUGHES na kampuni ya New Holland na kufanyika wilayani humo.

Mollel alisema kilimo chochote kiwe cha mpunga au mahindi kinapaswa kufuata kanuni za kilimo bora ikiwemo kutumia matrekta badala ya jembe la mkono kwenye kulima, kupanda vitalu vya mpunga na kisha kuupandikiza shambani, kuweka mbolea ya kukuzia na kisha kuvuna vizuri ikiwezekana kwa mashine na kuokoa upotevu wa chakula unaotokana na uvunaji usiofaa.

Alifafanua kuwa mkulima anayelima kilimo bora kwa kutumia pembejeo za kilimo hupata gunia 25-30 za mpunga kwa hekali moja tofauti na mkulima anayetumia jembe la mkono bila pembejeo ambaye hupata gunia 3-5.

Mollel alisema ni wakati sasa umefika wakulima wakatumia pembejo za kilimo ili kulima kilimo chenye tija kwa kupata mazao ya chakula na biashara na hivyo kuwa na maendeleo endelevu kwa njia ya kilimo.

Naye Afisa Mahusiano wa benki ya NMB Tawi la Kilombero Monica Kitilya ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya mpunga ikiwemo bonde la Kilombero ili kufanya kilimo katika maeneo mengi kuwa cha uhakika na chenye kukopesheka.

Kitilya alisema wakulima wengi wa mpunga kwenye bonde hilo wamekuwa wakikosa fursa za kukopesheka kutokana na kulima kilimo cha kutegemea mvua ambacho hakina uhakika.

Alisema sera za benki hiyo ni kutoa mikopo kamili kwa wakulima waliopo katika mifumo ya umwagiliajii na kwa wale walio nje ya mfumo huo benki inatoa mikopo katika hatua ya uvunaji pekee.


Awali mmoja wa wakulima waliopata mafunzo hayo Moshi Mgokeli aliishukuru kampuni hiyo kwa kushirikiana na Serikali kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewafanya kuona umuhimu wa matumizi ya pembejeo za kilimo kwa sababu wasipofuata kanuni bora za kilimo hujikuta wakipata gunia 4 hadi 5 za mpunga kwa hekali moja.

Hivyo aliziomba taasisi za kifedha kuwapatia mikopo itakayowainua na kujikita kwenye kilimo bora kwa kufuata kanuni za kilimo na hivyo kupata mazao mengi na mengine kuyaingia kwenye biashara na kutatua changamoto za kiuchumi kwenye Maisha kama vile kulipia karo za Watoto mashuleni.


Naye Kaimu Afisa kilimo halmashauri ya mji Ifakara Saida Selemani aliwashauri wakulima wa kilombero kutokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyopo duniani kuona muhimu wa kutumia pembejeo na teknolojia za kisasa za kilimo ikiwemo matrekta. 


Alisema kwa sasa kilimo cha jembe la mkono cha kutegemea mvua hakina nafasi katika kuleta mapinduzi ya kilimo na kuwataka kulima kilimo chenye tija.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post