POLISI YAKANUSHA TAARIFA ZA KUTEKWA WATOTO 12 ULANGA


 Na Christina Haule, Morogoro

JESHI la polisi mkoani hapa limekanusha taarifa za utekwaji wa Watoto 12 wa shule ya awali ya kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tarafa ya Mahenge Wilayani Ulanga mkoani Morogoro


Akizungumza na vyombo vya Habari Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amesema mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu taarifa zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa Watoto hao walitekwa na mwanamke mmoja na kuwapakia kwenye gari na kudai kuwa mwanamke huyo tayari ameshakamatwa na jeshi la polisi jambo ambalo sio kweli.

Kamanda Mkama amesema taarifa hizo ni za uongo ambapo baada ya kuona zinasambaa walilazimika kufanya uchunguzi hadi kwenye shule husika na kubaini kuwa siku ya tukio lilipoanza kusambazwa Watoto hao walikuwa 44 darasani kati ya wanafunzi 46 waliopo kwenye kituo hicho.

Hivyo aliwataka wananchi kuzipuuza taarifa hizo ambazo ni za uzushi na zilipikwa ili kuchafua na kuleta taharuki kwa lengo la kuvuruga hali ya usalama na amani ya wilaya na mkoa.

Aidha Jeshi la polisi linawataka wananchi kuacha tabia ya kutumia taarifa za kuzusha na kuleta taharuki kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu kufanya hivyoni kosa na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post