TBS YAWATAKA WAFANYABIASHARA WA VIPODOZI KUSAJILI BIDHAA ZAO KABLA HAZIJAINGIA SOKONI

Kaimu Meneja wa usajili wa bidhaa TBS Bi.Noor Meghji akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12,2024 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam

*********************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wa bidhaa za Vipodozi nchini wametakiwa kufanya maombi ya  usajili wa bidhaa  hizo kabla ya kuziingiza katika soko la ndani kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda usalama kwa watumiaji wa bidhaa hizo.

Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam leo Aprili 12,2024 na Kaimu Meneja wa usajili wa bidhaa TBS Bi.Noor Meghji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa elimu kwa Umma kuhusu taratibu za uingizaji bidhaa za vipodozi sokoni.

Bi.Meghji amesema bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kawaida  hupatiwa cheti kinachoidhinisha ubora wa bidhaa hiyo kutoka Shirika la Viwango,ambapo kwa mfanyabiashara anayetaka kuagiza bidhaa za vipodozi,anatakiwa kuomba usajili wa bidhaa hiyo kupitia mfumo unaopatikana kwenye tovuti ya TBS ili zikaguliwe na kujiridhisha ubora wake kabla ya kuingia sokoni.

Aidha Bi.Meghji ameeleza kuwa atakayesajili bidhaa hizo za kutoka nje,kwa mujibu wa Sheria anatakiwa pia kusajili jengo ambalo linatumika kuzihifadhi ambapo itasaidia kurahisisha utunzaji wake ili kuhakikisha usalama kwa watumiaji.

Pamoja na hayo Bi.Meghji amebainisha  umuhimu wa kufanya usajili ambapo inawapatia fursa ya kuangalia viambata ambavyo vimewekwa kwenye vipodozi hivyo na kufanya uchunguzi endapo vipodozi hivyo vinakidhi  matakwa ya viwango na kutoa usajili utakodumu kwa miaka mitano.

Kwa Upande wake, Afisa Viwango (TBS) Bw.Alexander Mashalla amesema ikiwa vipodozi vitazalishwa bila kufuata matakwa ya viwango nchini vitasababisha madhara kwa wananchi ambapo viwango vinavyoandaliwa na TBS vimeweka masharti kuzuia utumiaji wa viambato vyenye sumu.

Aidha  Bw.Mashalla ametoa rai kwa wazalishaji na watumiaji wa vipodozi kutokupuuzia kufuata masharti ya viwango vilivyowekwa ili wasipate madhara ya magonjwa ya kansa,aleji kwenye ngozi,na kusababisha ngozi kuwa laini kupitiliza ambapo inachangia mambukizi ya magonjwa mengine.

TBS imeaadhimia kulinda afya za walaji na watumiaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za vipodozi kwa kuandaa viwango ili kukidhi matakwa ya ubora kwa lengo la kulinda afya za watumiaji.
Kaimu Meneja wa usajili wa bidhaa TBS Bi.Noor Meghji akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12,2024 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam
Afisa Viwango (TBS) Bw.Alexander Mashalla akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12,2024 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post