MULEBA WAOMBEA TAIFA LA TANZANIA KUELEKEA MIAKA 60 YA MUUNGANO..DC DKT. NYAMAHANGA ASISITIZA ,AMANI , UMOJA NA MSHIKAMANO

Wananchi,watumishi na viongozi wa dini wakiwa kwenye ibada maalum ya kuliombea Taifa,Viongozi wa Kitaifa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano
Mwinjilisti wa kanisa  la Kiinjili la Kirutheri Tanzania Felician Mathias wakati akiomba katika ibada maalum ya kuliombea Taifa
Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt Abel Nyamahanga akizungumza na wanachi,Viongozi wa dini na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati wa ibada maalum ya kuliombea Taifa
Sheikh Nurani Amri akiomba wakati wa ibada maalum ya kuliombea Taifa,Viongozi wa Kitaifa ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano

Na Mariam Kagenda _Kagera

Katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wananchi wilayani Muleba mkoani Kagera wamehimizwa kuendelea   kudumisha mila, desturi, umoja na mshikamano kwa mustakabali wa nchi ya Tanzania.



Mkuu wa wilaya ya Muleba Dkt
 Abel Nyamahanga amesema hayo leo wakati wa ibada maalum  ya kuliombea  Taifa na viongozi sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya muungano kati ya  Tanganyika na Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba .



Dkt Nyamahanga amesema kila mwananchi anatakiwa  kuendelea kuuheshimu Muungano huo kwa kudumisha amani iliyopo kwani viongozi waliohasisi jambo hilo waliamini kuwa umoja ni Nguvu .


Amesema kuwa jambo lililofanywa na viongozi  Katika kuchanganya udongo wa pande mbili tafsiri yake ilikuwa ni kuunganisha watanzania hivyo hakuna mtu atakayeweza kuwatenganisha kwa namna yoyote  kila mmoja anatakiwa kuendelea kuuheshimu Muungano ili uweze kudumu .


Ameongeza kuwa Muungano huo ndiyo unawapa heshima watanzania,unawapa heshima ya uhuru Watanzania na unayapa hadhi mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwamba wote ni familia moja  kwani ukienda Zanzibar unawakuta Watanzania wanafanya Biashara na ukija Tanzania unamkuta Mzanzibar anafanya biashara na hayo ndiyo mafanikio ya Muungano.


Kwa upande wao baadhi ya viongozi walioongoza ibada hiyo Shekhe Nurani Amri pamoja na Mwinjilisiti kutoka kanisa la Kiinjiri la Kirutheri Tanzania wilaya ya Muleba Felician Mathias wamewahimiza Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi waliopo madarakani wakati wote wanapopata nafasi ya kuomba ili waweze kuendelea kuwaongoza katika misingi inayompendeza mwenyezi Mungu.


Kabla ya ibada hiyo viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba , Watumishi pamoja na wananchi wa wilaya hiyo waliungana kwa pamoja kufanya usafi katika kituo cha afya Kaigara kilichopo wilayani humo ambapo kesho watashiriki katika michezo mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post