‘’MSIWAHUDUMIE WANANCHI KWA HALI ZAO’’-NAIBU WAZIRI PINDA

Waziri Mkuu Mhe, Kasim Majaliwa Majaliwa akiwasili kufungua mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.

*************************

Na Munir Shemweta, RUANGWA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuacha kuwahudumia wananchi kwa kuangalia hali zao na badala yake watende haki katika kutoa huduma.

Mhe Pinda ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Machi 2024 wilayani Ruangwa mkoani Lindi wakati wa kufunga Mkutano wa Wadau katika ngazi ya wilaya kujadili mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini, mkutano uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kasim Majaliwa Majaliwa.

‘’Katika kutoa huduma hizi tusiangalie hali ya mtu tuangalie haki ya mtu na huo ndiyo msingi wa wizara ya ardhi kwa kuwa hapa Ruangwa leo vinaitwa vijiji kesho ni mji hivyo wanaweza kuja watendaji wengine wakaanza kusema michoro haikuzingatiwa kwa kuangalia hali ya mtu, hiyo haiwezekani’’. Alisema Mhe, Pinda

Amewaambia watendaji hao wa sekta ya ardhi kupitia mkutano wa wadau kuwa, pale wanapopokea mwekezaji sehemu ambayo tayari ina mipango ya matumizi ya ardhi basi taratibu zizingatiwe na kusisitiza pasiwe na suala la kuvamia vijiji vilivyowekewa mipango ya matumizi.

‘’Tukishafika katika kijiji kuna kamati ya ardhi, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kuuza ardhi ya kipande cha kijiji lazima mkutano mkuu uitwe kwa kushirikisha na wale wote walioshiriki kupanga mpango wa matumizi ya ardhi’’ alisema Mhe Pinda.

Mbali na suala hilo Mhe, Pinda alielezea suala la ushirikishwaji wananchi kwenye kupanga mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji ambapo amesema ushirikishwaji wadau ni kipaumbele namba moja kwenye mradi wa uboreshaji miliki za ardhi na ushirikishwaji huo unaanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa lengo la kuwafanya wananchi kuuelewa mradi ipasavyo.

Akitolea mfano wa wilaya ya Ruangwa, Mhe, Pinda amesema ushirikishwaji katika wilaya hiyo umelenga kupata taarifa ya utekelezaji katika wilaya na baadaye wadau kutoa maoni yao.

Katika mkutano huo wa siku moja wa wadau, mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kasimu Majaliwa Majaliwa alizindua Ripoti ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji katika wilaya ya Ruangwa na kutoa vyeti 18 vya ardhi ya vijiji.

Waziri Mkuu aliwaeleza washiriki wa mkutano huo wa wadau kuwa, nia ya serikali ya Tanzania ni kupima ardhi yote ili wananchi wakiwemo wana vijiji waweze kuitumia kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi.

Aidha, amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kushirikiana na wizara ya ardhi kufanikisha mradi wa uboreshaji milki za ardhi nchini.

Mradi wa Uboreshaji Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa unalenga kuvifikia vijiji vyote kwa lengo la kuvihakikishia vinapata mafanikio.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza katika mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.
Waratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa wakiwa katika mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.
Waziri Mkuu Mhe, Kasim Majaliwa Majaliwa akimkabidhi Cheti cha Kijiji kwa mmoja wa viongozi wa vijiji wakati wa mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.
Waziri Mkuu Mhe, Kasim Majaliwa akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.
Waziri Mkuu Mhe, Kasim Majaliwa Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa vijiji mara baada ya kuwakabidhi vyeti wakati wa mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.
Waziri Mkuu Mhe, Kasim Majaliwa Majaliwa, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma wakipiga makofi wakati wa mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024.
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa wadau kuhusu utekelezaji Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika wilayani Ruangwa mkoa wa Lindi tarehe 22 Machi 2024. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post