WASANII WAASWA KUZINGATIA MAADILI YA KITANZANIA KATIKA KAZI ZAO

Na Rose Ngunangwa, Bagamoyo

Wasanii nchini Tanzania wameaswa kutumia vema uhuru wa kutoa burudani kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa kitanzania ili kuwalinda watoto na vijana dhidi ya mmomonyoko wa maadili.

Wito huu umetolewa leo mjini Bagamoyo na bwana Peter Saimon afisa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na UNESCO ili kujadili mpango mkakati wa Mkataba wa Kimataifa wa UNESCO wa mwaka 2005 katika nyakati hizi za kidijitali.

“Uhuru wa kufanya kazi za sanaa haumaanishi msanii kuvaa nusu utupu la hasha bali kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kitanzania, “ alisema bwana Saimon.

Alisisitiza pia umuhimu wa watanzania kuanza kuitambua sanaa kama sekta yenye mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi badala ya kuichukulia tu kama burudani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tamasha la Kimataifa la Zanzibar bwana Martin Mhando alisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo rafiki ya ukusanyaji wa kodi kwa wasanii ikiwemo kuhakikisha wasanii wanapata malipo stahiki wanapopandisha kazi zao kwenye mitandao ya kijamii kama facebook na mingineyo.

Kikao kazi hicho kimewakutanisha wadau wa sekta ya Sanaa na ubunifu kwa lengo la kupitia mpango mkakati wa Mkataba wa Kimataifa wa UNESCO wa mwaka 2005 ili uweze kuendana na mazingira ya kitanzania hususani nyakati hizi za kidijitali.

Moja ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuhakikisha mkataba huu unafasiliwa kwa lugha ya Kiswahili ili maudhui yake yaweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Mkataba huu unalenga kusaidia kutengeneza mifumo endelevu ya kusimamia masuala ya utamaduni ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma za kiutamaduni na kuweka mazingira rafiki ya wasanii kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kufanya kazi za kiutamaduni.

Malengo mengine ni pamoja na kujumuisha masuala ya kiutamaduni kwenye mipango ya Maendeleo endelevu ili kukuza haki za binadamu na uhuru pamoja.

Kikao hiki kinawajumuisha wadau kutoka wizara za sanaa za bara na visiwani, COSOTA, BASATA, BAKITA, Bodi ya Filamu Tanzania, TASUBA, COSOZA, BAKIZA , Shirikisho la Wasanii wanawake Tanzania, NATCOM, sekta binafsi na waandishi wa habari.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments