SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UUZAJI POMBE, MATUNDA KUPAMBANA NA KIPINDUPINDU MULEBA

 
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga 

Na Mariam Kagenda _ MULEBA

Serikali wilayani Muleba Mkoani Kagera imepiga marufuku uuzaji wa pombe za kienyeji pamoja na wazazi kuwatembelea wanafunzi shuleni katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ili kuweza kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga amesema hayo leo hii wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema kuwa tayari ugonjwa huo umeishaenea katika Wilaya hiyo hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari.

Dkt. Nyamahanga amesema kuwa pia wamepiga marufuku uuzaji wa matunda yaliyomenywa kwa kipindi hiki huku wakitakiwa kushiriki kufanya usafi kikamilifu ili kujikinga na ugonjwa huo wa kipindupindu katika Wilaya ya Muleba.

Aidha amesema kuwa dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni kutapika, kuhara pamoja na mwili kuishiwa nguvu hivyo endapo mtu akihisi kuwa na dalili za ugonjwa huo  anatakiwa kufika kwenye kituo cha afya ili aweze kupata matibabu haraka.

Kwa upande wake Afisa Afya Wilaya ya Muleba Bw. Johanes Mtoka amesema kuwa tangu ugonjwa huo ulipotiwe tarehe 14 Desemba 2023 jumla ya watu sita wamefariki  huku wagonjwa wakiwa 146 ambapo wametibiwa na kuruhusiwa .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments